Friday, 27 May 2016

KAMA MZAZI: Uko wapi mwarobaini wa mmomonyoko wa maadili?TANGU zama za kale wahenga walikuwa na misemo yao iliyotumika kutoa onyo na mafunzo mbalimbali kwa jamii. Misemo hiyo ipo ya zamani bila kusahau inayoibuka siku hizi ikiwa na nafasi muhimu katika jamii.
Mmoja wa semi hizo ni ule unaosema ‘Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji.’ Maana kubwa ya usemi hii ni kwamba kama unashuhudia mwenzio ananyolewa ni vizuri wewe ambaye uko katika foleni ya kusubiri kunyolewa, utie maji, hatua itakayozifanya nywele zako ziwe laini ili wakati wako ukifika wa kunyolewa hatua hiyo iwe imeshafanyika kiasi kwamba hutosikia mikwaruzo au maumivu kama mwenzio ambaye alinyolewa bila kutia kwanza maji.

Kona hii ya Kama Mzazi, hapo inafahamu kwamba ni vizuri mtu akajiandaa mapema kama ana mpango fulani anaotaka kuutekeleza ili wakati ukiwadia kwa ajili ya utekelezaji wake asipate vikwazo.
Matukio ya ukosefu wa maadili yanazidi kuongezeka siku hadi siku katika jamii yetu kiasi cha kutoa ishara kwamba Watanzania wameanza kuzoea na kuona kuwa ni jambo la kawaida katika maisha yao ya kila siku.
Hali hii si njema kwani inaweza ikapindukia kuwa utamaduni na vizazi vikaanza kurithishana. Siku hizi kila kukicha hukosi kusikia katika vyombo vya habari vitendo vya ubakaji, ulawiti, ukatili wa kijinsia au ngono zembe tena si kwa watu wazima tu bali hata wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Yapo matukio ya wanafunzi kushiriki ngono na akinadada poa kwa malipo ya Sh 2,000, yapo matukio ya ndoa za utotoni, kuacha shule kwa kupata ujauzito na hata walimu wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu kufanya mapenzi na wanafunzi wao ambao kimsingi wao ni walezi wao, sawa na wazazi wao.
Katika tasnia ya habari tunaweza kusema hizi ni habari zinazopamba habari za kijamii katika taifa letu kila kukicha kama vile tunafanya kampeni dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi au malaria. Hivi kama hali ikiendelea hivi kwa miaka mingine 10 ijayo, Tanzania yetu itakuwa ni jamii ya aina gani?
Mmomonyoko huu mkubwa wa maadili unaotukabili na kujichimbia kwenye jamii yetu tutaudhibiti vipi? Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia, afya na kijamii mko wapi? Narudia usemi wetu wa awali kwamba Ukiona mwenzako ananyolewa, wewe tia maji.
Hapa Kama Mzazi inamaanisha kwamba mmomonyoko huu utamgusa kila mmoja kwa nafasi yake kama mzazi, mlezi, mwalimu au mwananchi tu wa kawaida. Wakati umefika sasa wa wataalamu wetu waliobobea katika sekta na nyanja mbalimbali kuketi kwa pamoja na kufanya utafiti na uchambuzi wa jinsi ya kuweza kukabiliana na kadhia hii kwa muda mfupi na pia kwa muda mrefu kama jamii kwa lengo la kurejesha ustawi na ustaarabu wa jamii yetu.
Hakuna kinachoshindikana kama nia thabiti ya kukabiliana na tatizo hili itakuwepo. Wataalamu wakishapata kiini na namna ya kukwamua basi bila shaka serikali, wananchi na wataalamu kwa ujumla wao washikamane na kuingia vitani dhidi ya mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu.
Umoja ni nguvu na katika hili tusifanya mzaha. Tuliwekee mikakati ya uhakika na uhalisia itakayotutoa katika kadhia hii ambayo kwa bahati mbaya bado hatujapata njia bora na ya kudumu ya kukabiliana na tatizo hili.
Jambo moja la kutufariji ni kwamba kila mmoja wetu sasa analiona na kulishuhudia hili na kwamba hakuna ubishi kwamba tuna tatizo. Kujua tatizo ni hatua moja mbele ya kutaka kulitafutia ufumbuzi. Tushikamane tujinasue.