Ingawa miaka ya nyuma masafa yalikuwa na taathira katika uhusiano na maingiliano ya wanadamu, leo mawasiliano ya wanadamu yameenea na kuwa na kasi ya juu kutokana na kuenea intaneti na mitandao ya kijamii katika kila kona ya dunia. Tunashuhudia kuwa, watu walio katika maeneo tafauti ya umbali wa maelfu ya kilomita wanawasiliana kwa kasi ya sekunde chache kwa gharama ya chini sana na hata wakati mwingine pasina kutoa malipo kwa kutumia mitandao ya kijamii. Karibuni katika makala yetu ya leo ambapo tutaendelea kujadili sifa za kipekee za mitandao ya kijamii.
Kutokana na mvuto wake maalumu mitandao ya kijamii imeweza kuwavutia watu wengi wa matabaka mbali mbali ya jamii. Kutaka kuwa na uhusiano zaidi na wanaadamu wengine na kushiriki katika masuala ya kijamii ni moja kati ya mahitajio muhimu ya mwanadamu.
Nukta hii ndiyo iliyopelekea idadi kubwa ya watu kuvutiwa na mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii kwa njia ya intaneti. Pamoja na hayo tunashuhudia watu wakiitumia teknolojia hii visivyo. Kutumia wakati mwingi kupita kiasi katika mitandao ya intaneti ni tabia ambayo imetajwa kuwa ni ‘uraibu wa intaneti.’ Wataalamu wamebaini kuwa uraibu huu huwa na madhara mengi kwa mtu binafsi na jamii na huathiri vibaya kiwango cha ukuruba na mahaba katika familia, jamaa na marafiki.
Familia ni taasisi muhimu zaidi ya kijamii na hupaswa kuwa ni mazingira ya kuinukia mwanadamu atakayekuwa mwenye manufaa katika siku za usoni. Kwa msingi huo jamii ambayo ina familia salama zilizojaa mahaba na ukuruba wa wanafamilia huwa na mustakabali uliojaa nuru.
migogoro huwa pale unapobaini mwenzi wako amewasiliana na mtu ambaye unahisi anamahusiano naye. |
Ninakumbuka mama mzazi ambaye alikuwa akisema mwanae huona haya. Hapo akaamua kuelekea kwa mwanasaikolojia amsaidie kutatua tatizo hilo. Walipofika hapo akaambiwa kuwa katika kikao kijacho mtoto huyo alete michoro ya kitoto ambayo huichora. Kulikuwa na nukta iliyomvutia daktari katika michoro hiyo. Katika michoro hiyo baba hakuonekana. Daktari akamuuliza mama iwapo ametengana na baba yake mtoto. Mama akajibu kwa kustaajabu na kusema, “La Bw. Daktari, sisi tunaishi pamoja kwa muda wa takribani miaka 10 sasa.” Daktari akahoji, basi ni kwa nini binti yako hajamchora baba katika michoro yake? Mama akajibu: “Nasikitika kusema kuwa, mume wangu kila anaporudi nyumbani, baada ya kupumzika kidogo huketi mbele ya kompyuta yake na wala hamzingatii huyu mtoto. Wakati binti yangu anapoelekea alipo baba yake, yeye humzomea na kumuambia asimsumbue kwani atamvurugia kazi zake. Si tu kuwa hamzingatii binti yangu bali mimi pia kwa miaka mingi amekuwa hanionyeshi mahaba na hivyo najihisi mchovu sana.”
Kisa hiki yamkini kikawa pia katika maisha ya watu wengi wanaoishi katika karne hii. Si kinababa tu bali pia kinamama nao pia hutumia wakati wao mwingi wakiwa katika mitandao ya kijamii kwenye intaneti. Hali huwa mbaya kiasi kwamba mtu anaweza kukaa masaa kadhaa kwenye intaneti pasina yeye kujua muda unapita kwa kasi na anapotizama saa anagundua kuwa amekuwa katika intaneti kwa muda mrefu sana.
Uraibu wa intaneti na mitandao ya kijamii hupelekea kuvurugika kwa kiasi kikubwa uhusiano miongoni mwa wana familia.
Muda unaopaswa kupitishwa katika mahaba na mapenzi baina ya wana familia na kutatua matatizo ya kifamilia kupitia mazungumzo na ukuruba hivi sasa hutumiwa katika mambo yasiyo na umuhimu kama vile kutuma maoni kuhusu picha katika mitandao ya kijamii au kuchangia mijadala ya mitandao hiyo ya kijamii katika intaneti. Wakati mwingine yanayojadiliwa katika mitandao hiyo huwa ni masuala ya udaku, usengenyaji n.k mambo ambayo ni kinyume na maadili bora ya mwanadamu. Wakati mwingine kina mama hujishughulisha na mitandao ya kijamii katika intaneti kiasi cha kughafilika na masuala muhimu ya nyumba na malezi ya watoto. Hali hii hupelekea mume na watoto pia kutoridhika. Nukta nyingine ambayo wataalamu wamefikia natija ni kuwa, watu ambao hupitisha wakati wao mwingi wakiwa katika mitandao ya kijamii huwa wanaficha ukweli kuhusu maisha yao na wakati mwingi hufunika matatizo yao. Nukta hii hupelekea wale walio na shida katika maisha kupoteza matumaini maishani.
Pamoja na hayo, haina maana kuwa teknolojia mpya za kisasa za mawasiliano ni haribifu. Kama ambavyo tumesisitiza mara kadhaa, kwa nafsi yake, intaneti na teknolojia zingine za mawasiliano si haribifu, kile chenye matatizo ni utumizi usio sahihi ambao humletea mwanadamu madhara.
kuchati hupunguza uangalizi wa familia. |
Na kama tulivosema matatizo hayo ni kama vile kutengana kimahaba na kihisia wana familia na hilo hupelekea kutikisika au hata kusambaratika familia. Aidha mitandao ya kijamii huandaa mazingira ya kuwa na uhusiano na watu ambao hawaakisi uhalisia wa mambo katika jamii. Hii ni kwa sababu aghalabu ya wanaotumia mitandao hii ya kijamii huwa hawapendi kuanika masaibu yao bali wengi huonyesha mazuri tu yanayojiri katika maisha yao na kwa njia hiyo kuibua hisia bandia miongoni mwa watumizi wengine wa mitandao hiyo. Hii ni katika hali ambayo iwapo wangezungumza au kukutana au kutembeleana wangeweza kujuliana hali na kusaidiana katika kutatua matatizo yao.
Aidha wataalamu wanaamini kuwa uhusiano wa watu wa jinsia mbili tafauti huanza haraka sana kupitia mitandao a kijamii kama vile facebook na twitter. Uhusiano kama huu huwa na madhara makubwa kwa vijana kwani yamkini ukaishia katika mahusiano haramu. Aidha kwa wanandoa, uhusiano wa kiintaneti wa watu wa jinsia mbili ambao ni ajinabii yamkini ukawa mwanzo wa kuvuruga ndoa. Kuna baadhi ya wanandoa ambao hudhani kuwa kuwa na uhusiano na mwanmke au mwanamume ajinabi katika intaneti au mitandao ya kijamii ni jambo lisilo na madhara au si dhambi na hivyo uhusiano huo hauhesabiwi kama hiana au usaliti katika ndoa. Lakini uchunguzi umebaini kuwa uhusiano wa wanawake na wanaume katika intaneti huwa hatua ya kwanza ya kuelekea katika madhambi makubwa na usaliti katika ndoa.
Kupata pigo mahaba na ukuruba wa kifamilia na kuzorota uhusiano mwema baina ya wanandoa ni mambo ambayo huwa na athari mbaya sana kwa jamii.
Baadhi ya watoto wambao huinukia katika familia zenye migogoro na misuguano hukumbwa na matatizo ya kisaikolojia katika siku za usoni na jambo hilo huathiri uhusiano wao wa kijamii. Wataalamu wa kidini wanasema kuimarishwa mahaba na mapenzi miongoni mwa wana familia huzuia kuporomoka familia.
Wataalamu hao wanasisitiza kuwepo mazingira mazuri ya mazungumzo na kubadilishana maoni katika familia. Kwa msingi huo wanandoa wanapaswa kuchukua tahadhari na kuhakikisha kuwa mitandao ya kijamii katika intaneti haiwi chanzo cha kupungua mahaba na uhusiano katika familia.
Kwa hivyo hapa tunafikia natija kuwa kinachopaswa kufanyika ni utumizi sahihi wa teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba teknolojia hii hasa intaneti na mitandao ya kijamii inapaswa kutumiwa kuimarisha uhusiano wa kifamilia.
TUTUMIE KWA MALENGO CHANYA.