Wednesday, 13 July 2016

NAFASI YA BABA KATIKA MALEZI NA MAENDELEO YA MTOTO !!

Kama ni kweli kuwa mtoto hawezi kuzaliwa bila ya baba na mama basi hawezi kukamilika bila ya baba na mama. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi kuhusu mama na nafasi yake kwa mtoto. Mama anao wajibu wake kama mama na ndio maana ni mama na hawezi kuwa baba. Mama anaweza kuyafanya mambo mengi kama baba lakini hawezi kuwa na ladha ya baba. Hivyo basi nafasi ya baba ni muhimu kwa malezi na makuzi ya mtoto. 
Na nafasi ya baba na umuhimu wake ni zaidi ya pesa anazotoa kwa matumizi ya familia na huduma kwa mtoto. Baba anayo nafasi kubwa sana kwa mtoto katika kukua kwake na hata maendeleo yake. Malezi na maendeleo ya mtoto aliyekosa baba huwa na mapungufu kwa mtoto kijamii,kisaikolojia,kibaolojia,kiakili, kiroho na hata kimaumbile.

kumbeba mtoto humjengea mtoto uwezo wa kujua wewe kama mzazi unaupendo kwake.
Bila baba maisha ya mtoto hukosa mengi ambaye humfanya mtoto kutokamilika. Mtoto bila baba hatakamilika hata awe na umri mkubwa kivipi. Na ikumbukwe kuwa sio kila mtu anayeonekana ni mtu mzima amekamilika kimakuzi na muda mwingine wengine hushindwa kuwa baba kwasababu hawakupata malezi ya baba, hivyo hawakukamilika. Baba ni ukamilifu wa mtoto. Kama mtoto hawezi kuzaliwa bila baba na mama basi hawezi kukamilika bila malezi ya baba na mama. Mtoto anamhitaji baba. Mwanaume anapokuwa baba dunia yake hubadilika, na yeye huwa zaidi ya mume wa mtu – kwasababu – anaingia katika wajibu wa kulea na kumwongoza mtoto.
Na katika familia wababa wengi huonekana kimwili zaidi, lakini moyoni wengi wao huwa hawapo - kwani wengi huwa mbali na watoto kiasi ambacho huonekana kama wasaidizi tu katika kumlea mtoto na kujisahau kuwa , mama hawezi kuwa badala ya baba na wao kama wakina baba wanao wajibu mkubwa zaidi, mbali na kuhudumia familia , pia wanahusika sana katika makuzi ya watoto wao kama wababa.
Baba ni ufunguo wa mtoto kupata ujasiri wa maisha, sio kwamba mama hawezi kuyafanya hivyo bali mama hufanya kwa nafasi yake, lakini ladha ya kibaba inapatikana kwa baba mwenyewe. Baba anahusika sana katika malezi na makuzi ya mtoto , hasa katika mambo yafuatayo;
a) Baba ni Nguzo ya Kujenga Mahusiano Mazuri na Mama wa watoto: Kipimo kikubwa cha ubaba si uwezo wa kifedha tu peke yake, si umbile na wala sauti yake bali ni uwezo wa kutengeneza mfumo mzuri wa mahusiano kati ya yeye na mke wake. Baba ni kichwa cha familia, ni mhusika mkuu anayetakiwa kutengeneza mfumo wa familia. Ni mhusika mkuu anayetakiwa kujenga nguzo za ndoa kama amani,upendo,maendeleo na uwajibikaji. Ndoa ina mengi lakini ni baba ndio mwenye mengi ya kuifanya ndoa ikae sawa. Kwa kuyafanya hayo huweza kujenga picha nzuri kwa watoto na hata katika kukua kwao.
b) Kuwa na muda mzuri na watoto: Akili ya mtoto mdogo hutafisiri na hutambua mapenzi kwa muda mtu anaochukiwa kuwa na mtoto huyo. Kwa bahati mbaya katika jamii yetu muda wa baba katika familia huwa ni mchache sana; hata kama dunia ipo busy kiasi gani baba anatakiwa kujua kuwa muda wake na familia ni wa maana sana katika maisha ya watoto. Watoto huweza kujifunza mengi sana kwa uwepo wake na baba pia anaweza kuyajua mengi ya watoto wake na hata kuyarekebisha au kuyaboresha.
c) Baba ni mlinzi na mhusika mkuu wa Familia:
 Baba ni kiungo muhimu katika familia, ni mhusika mkuu katika kuhudumia familia na hata ulinzi wa watoto. Kipimo cha mwanaume si uwezo wake wa kimwili bali ni uwezo wa kutoa huduma katika familia na hata kuwa mhusika mlinzi wa watoto katika usalama wao kimaadili na hata kitabia. Hata kama baba hana uwezo wa kifedha bado anayo nguvu ya kibaba katika hili. Si kwamba mama hawezi kuwalinda watoto,lakini hawezi kufanya kama baba, yatupasa wote tufahamu ya kuwa; hakuna mama kama baba na wala hakuna baba kama mama.
d) Baba ni mwalimu wa familia:
 Maisha yana mengi ya kujifunza, mtoto ni kiumbe asiye na kosa. Hupokea na kujifunza chochote atakachofundishwa. Ni wajibu wa baba kujua mtoto ajifunze nini katika maisha, ajue nini na aishi vipi. Baba amepitia mengi na katika hayo baba anaweza kuzungumza na mtoto katika lugha ya kawaida ili kumfunza mtoto katika hayo. Baba ni mwalimu wa maisha kwa mtoto. Baba ni zaidi ya kocha wa mpira katika maisha ya mtoto. Baba ni dunia ya mtoto.Hatima ya maisha ya mtoto katika makuzi,maisha,nidhamu na hata maadili ipo mikononi mwa baba. Baba ni mhusika mkuu na kisababishi kikubwa cha kwanini mtoto awe/ amekuwa jinsi alivyo. Baba ni ufunguo wa maisha ya mtoto.
e) Baba ni mfano wa kuigwa wa mtoto (role model) :
 Uhusiano wa baba na mtoto una maana kubwa sana. Baba ni chanzo cha kwanini mtoto hufeli au hufaulu , chanzo cha mtoto kujua au kutokujua. Maisha ya baba ni picha ya maisha ya baadaye ya mtoto. Tabia ya baba ya nje na ndani ya familia ni kioo cha mtoto. Yawapasa wakinana baba wote watambue kuwa: ‘Wao ni kioo cha familia, haswa kwa watoto’. Chochote kile anachofanya nje na ndani ya familia,vyovyote vile anavyoishi na watu wa nje na ndani ya familia na hata matumizi ya hela na kazi yake ndivyo anavyomjenga au kumbomoa mtoto.

Nahitimisha kwa kusema; kuwa baba si kuzaa tu , maana ingekuwa hivyo - hata wanyama wanazaa pia. Kuwa baba ni zaidi ya kuzaa; ni kuwa mhusika kwa kujua kabisa kuwa maisha ya mtoto yanaweza kutengenezwa au kuharibiwa kutokana na kuwepo au kutokuwepo kwa mwongozo kutoka kwa baba. Hivyo basi baba anayo nafasi kubwa sana katika malezi na maendeleo ya mtoto katika maisha yake, mtoto ambaye ndiye anayetegemewa kuijenga nchi yetu ya Tanzania.
Simameni basi wakina baba na mchukue nafasi zenu, wako wapi wakina baba ambao watasimama na mimi leo na kusema, tutashiriki kikamilifu katika malezi na makuzi, pia katika kulinda familia zetu na kuongoza watoto wetu kwa hekima, busara na upendo?
Tuwapende na kuwalinda watoto wetu.
SMGEO