By Tumaini Msowoya, Mwananchi 
Siyo kama zamani. Walau wanawake wanafurukuta na wameweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo za juu katika nchi.
Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, Tanzania inaadhimisha siku ya wanawake duniani wakati Makamu wa Rais akiwa mwanamke.
Wanawake wengine waliowahi kushika nafasi za juu na wanaoshika nafasi hizo ni Spika wa zamani wa Bunge, Anna Makinda, Naibu Spika wa sasa Dk Tulia Akson, pia wapo baadhi ya mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya.
Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 1995, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza idadi ya wanawake waliokuwa wakijitokeza kuwania uongozi kwenye uchaguzi mkuu ilikuwa ndogo.
Ni wanawake nane tu waliojitosa majimboni ambao walishinda ubunge. Wanawake 37 walipata ubunge kupitia nafasi za viti maalum na hivyo kufanya idadi ya wanawake bungeni kuwa 45 kati ya 269 waliochaguliwa, sawa na asilimia 16.
Hata hivyo idadi hiyo iliendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 36 mwaka 2010.
Muamko wa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi imeongezeka mara dufu mwaka jana, baada ya baadhi yao kuamua kuwania urais, nafasi ya uongozi ya juu kabisa nchini.
Miongoni mwa wanawake waliopambana katika kuusaka urais ni Anna Mgwira aliyewania kupitia chama cha ACT-Wazalendo. Wengine akiwamo Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ally walioishia kwenye chaguzi za ndani ya CCM.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi anasema malengo ya millennia ambayo ukomo wake ulikuwa mwaka jana hayajaweza kufikiwa.
“Licha ya kuwa tumejihidi kupiga hatua, bado hatukuweza kufikia usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 wanawake kwa wanaume kwenye uongozi,” anasema.
Kukwama huko kumewalazimisha wanawake duniani kutengeneza malengo mengine mapya yenye kauli mbiu ‘50 kwa 50 ifikapo 2030, tuongeze jitihada.
Kilichowakwamisha
Wanaharakati wa masuala ya kijinsia nchini wanasema vipo vikwazo vingi vinavyokwamisha jitihada za wanawake kiuongozi.
Mwanaharakati wa TGNP kutoka mkoa wa Shinyanga, Fredina Said anasema rushwa, kashfa, mila potofu na ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa vikwazo vya kutofikia malengo.
“Uchaguzi uliopita niligombea udiwani wa kata ya Ukenyenge, wilaya ya Kishapu. Nilipambana kadri ya uwezo wangu lakini matumizi makubwa ya fedha na kashfa vilinirudisha nyuma,” anasema.
Anasema kinachoweza kuwasaidia wanawake ni wao wenyewe kuungana mkono na kutokubali kufedheheshwa kutokana na mfumo dume.
Mwanaharakati mwingine kutoka Mkoa wa Mbeya, Felista Kaisi anasema wanawake wenyewe ni kikwazo kikubwa kwa wenzao kufanikiwa.
wsababu ya mfumo dume kuwatesa kwa madai kuwa baadhi yao wamekuwa wakiwadharau wenzao na kuwaunga mkono wanaume.
“Utashangaa kipindi cha uchaguzi mwanamke anakuwa adui namba moja wa mwanamke mwenzake, hili ni tatizo ambalo litatufanya tuendelee kusota,” anasema.
Anasema kama wanawake watashindwa kuwaunga mkono wenzao, wanaume watapita katikati yao na kushinda.
Mbunge wa jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya(CUF) anasema bado kuna safari ndefu ya kuhakikisha wanawake wanaheshimiwa wanapowania uongozi.
Anasema licha ya kupambana usiku na mchana bado misukosuko ikiwamo kutukanwa, kudhalilishwa na kudhihakiwa imekuwa kikwazo kwa mwanamke kupata uongozi.
Sakaya ambaye alimshinda kwa mbinde, Waziri wa zamani, Profesa Juma Kapuya aliyeliongoza jimbo hilo kwa miaka mingi anasema kuna siku alilazimika kumuomba mume wake aueleze umma na kufuta maneno ya kashfa aliyokuwa akizushiwa.
“Nilitukanwa kiasi cha kuitwa malaya pale wapinzani wangu walipobaini nina nguvu, hata hivyo sikukata tamaa niliendelea kupambana na nikaungwa mkono na makundi mengi hasa vijana. Namshukuru mume wangu aliinuka kueleza kuwa nastahili,” anasema.
Anakiri kuwa bado zinahitajika nguvu za ziada ili kuweza kuyafikia malengo yaliyopangwa na hilo litawezekana kama wanawake wenyewe wataungana mikono. Mkurugenzi wa Kituo Cha Haki za Binadamu(LHRC), Hellen Kijo Bisimba anasema dhana potofu kuhusu harakati za kumkomboa mwanamke, pia zinachangia kurudisha nyuma malengo ya millennia.
Bisimba ambaye alikuwa miongoni mwa wanawake waliosafiri hadi Beijing kutafuta usawa wa kijinsia, anasema kutokata tamaa, kuacha hofu, kujituma na kujiamini kutawasaidia kufikia usawa wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA), Stella Jairos ambaye alikuwa miongoni mwa wanawake walioamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge anasema hakuna njia nyingine ya kufanikiwa, zaidi ya wanawake kuwa wamoja.
Hata hivyo anasema wanawake wenye ulemavu, wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi ikilinganishwa na wanawake wasio na ulemavu.
“Mwanamke mlemavu akigombea utasikia ‘huyu naye anataka uongozi? Atatuongoza nini wakati haoni? Tuna changamoto nyingi zaidi,” anasema.
Mikakati ya kufanikiwa
Afisa Mwandamizi wa Harakati na Ujenzi wa Nguvu za pamoja kutoka TGNP, Anna Sangai anasema mtandao huo na wanaharakati wengine, wanapambana kutengeneza mikakati itakayowasaidia wanawake kutambua nafasi na uwezo wao kwenye jamii, ikiwamo kisiasa.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanatambua uwezo wao, fursa na namna wanavyoweza kubadili sura ya mfumo kandamizi,” anasema.
Mgawanyo wa rasilimali kwa usawa ni miongoni mwa agenda zao katika kufikia mafanikio.
Anasema wanatarajia kuja na mikakati mipya ya kuwawezesha wanawake, kutambua nafasi na uwezo wao kisiasa.
“Tunawashirikisha wanawake kwenye mikoa yote kuona kuwa wanaweza na wanafaa kuwa viongozi. Tunachofanya ni kuwafundisha ujasiri wa kuthubutu,” anasema.
Aidha Sangai anasema ni wakati wa wanawake kupambana na mila na desturi zilizopitwa na wakati.
“Wanawake tunataka usawa wa kijinsia katika uongozi, yaani uwe 50 kwa 50 na hilo linawezekana,” anasema.
Siku 100 za Magufuli na usawa wa kijinsia
Liundi anasema licha ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, uteuzi wa ngazi mbalimbali za maamuzi uliofanyika hadi sasa haujazingatia usawa wa kijinsi.
Jambo hilo linawapa wasiwasi wanaharakati hao katika kufikisha malengo yao waliyojiwekea katika kupambana na mfumo dume ambao umechangia kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia.
Anasema kwa ujumla teuzi hizo kwa kiasi kikubwa hazikuzingatia usawa wa kijinsia.
“Kama wanaharakati wa masuala ya jinsia tuliguswa na uteuzi wa baraza la mawaziri na makatibu wakuu, tulitarajia kungekuwa na usawa wa kijinsia lakini hilo halikuzingatiwa,” anasema.
Anasema kati ya mawaziri na manaibu mawaziri 35, wanawake ni 9 pekee sawa na 25.7% huku wanaume wakiwa 26 sawa na 74.28%.
Anasema makatibu wakuu na manaibu wanawake walioteuliwa ni 10 pekee sawa na asilimia 20 tu huku asilimia 80 inayobakia ikishikiliwa na wanaume.
Anasema Tanzania ni nchi ambayo imeridhia mikataba na matamko mengi ya kimataifa yanayosisitiza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake hususan ushiriki wao katika ngazi zote za maamuzi kimataifa, kikanda na hata sera na miongozo ya kitaifa.
“Mfano ni Azimio na Mpango kazi wa Beijing, Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ukandamizaji na Dhuluma dhidi ya Wanawake, mkataba wa Usawa wa Jinsia wa SADC, pamoja na ule wa Maputo, hii yote inatulazimisha kujali usawa kijinsia,” anasema.
Kutokana na mikataba hiyo anamuomba Rais kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye teuzi zilizobaki.
“Tunaomba kumkumbusha Rais kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kwenye teuzi zake zilizobaki kwa sababu, usawa huo husaidia katika kuleta utawala bora,” anasema.
Pia anawataka mawaziri na viongozi wengine kuzingatia usawa wa jinsia katika shughuli zao wanazofanya za kila siku ili kuhakikisha kuwa mahitaji ya wanawake, watu wenye ulemavu, watoto, wazee na vijana yanazingatiwa katika kufanya maamuzi.