Friday 27 May 2016

JPM kaepusha ‘vita’- Makinda


SPIKA mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Anne Makinda amesema kuchaguliwa kwa Dk John Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano, kumenusuru Watanzania na machafuko yaliyokuwa yakielekea kutokea.
Huku akipongeza mtindo wa Magufuli kuweka nchi sawa maarufu utumbuaji majipu, ambao umekuwa ukikosolewa na viongozi wa Chadema, Makinda amesema machafuko hayo, yalikuwa yasababishwe na tofauti kubwa ya vipato vya wananchi baina ya masikini na matajiri.
Alisema hayo jana alipozungumza na wanahabari k
wenye mkutano wa kupitia utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (Sagcot), katika Kongani ya Ihemi inayohusisha mikoa ya Iringa na Njombe.
“Tungeendelea tulivyokuwa tunaendelea, hakika tungekuja kuuana kwa sababu wenye nacho waliendelea kupata zaidi na wasio nacho waliongezeka kwa kuwa watumwa wa wenye nacho,” alisema Makinda.
Kauli hiyo ya Makinda, imekuja wakati viongozi wa Chadema wakionekana waziwazi kutetea watuhumiwa wa matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali za umma ambao wamekuwa wakichukuliwa hatua na uongozi wa Rais Magufuli.
Utetezi huo ulianza kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mwanzoni mwa Februari mwaka huu, ambapo wakati huo alionya alichoita fukuza fukuza ya watumishi wa umma bila utaratibu, huku akiomba viongozi wa dini kumsaidia kukemea.
Baadaye alikuja kuungwa mkono na makada wa chama hicho, akiwemo aliyekuwa mgombea wa Urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye mbali na kuwatetea watuhumiwa hao, alishauri watuhumiwa hao kwenda mahakamani akidai Rais Magufuli anaongoza nchi kama mali yake binafsi.
Mamilionea bila kazi
Makinda katika mazungumzo yake ya jana, alisema bahati mbaya iliyokuwa ikilikumba Taifa ambayo mwenye suluhisho lake ni Rais Magufuli, ni baadhi ya matajiri kutoeleweka wanafanya kazi gani, lakini wakifikia mafanikio waliyonayo kutokana na kunufaika kijanjajanja na fedha za Serikali.
“Kuna watu walikuwa hawaeleweki wanafanya kazi gani, lakini ni mamilionea, baadhi yao ndio wale walikuwa wananufaika na mamilioni ya Serikali,” alisema.
Makinda alisema katika kuiweka nchi sawa katika nyanja mbalimbali, kila Mtanzania ataonja machungu yatakayokuja kuliponyesha Taifa mbele ya safari.
“Kutakuwa na magumu, wengi watasema aah huyo bwana mbona kabana hivi, lakini ni muhimu Watanzania wajue hii ni oparesheni kubwa itakayotuumiza wote, lakini mwisho wa yote Taifa na Watanzania tutapona,” alisema.
Aliwataka Watanzania waendelee kumuombea kwa Mungu Dk Magufuli ili aendelee kuwa na afya njema, busara na afanye kazi kwa kasi aliyoanza nayo hadi atakapomaliza awamu yake.
Wanaompinga
Wakati Makinda akitoa kauli hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Mbowe baada ya kukosa kuungwa mkono na viongozi wa dini aliomba wamkemee Rais Magufuli mwanzoni mwa Februari, alikuja kuungwa mkono na Lowassa.
Lowassa yeye alidai kuwa utumbuaji majipu umesababisha hali mbaya ya maisha kwa wananchi, kwa kuwa watumishi hao wa umma wameachishwa kazi. Mgombea huyo alienda mbali zaidi na kudai kuwa, anasononeshwa anapoona watu wanaachishwa kazi katika mashirika ya umma.
Mbali na Lowassa, Lissu ambaye mbali na kuwa mwanasheria wa Chadema, pia ni Waziri Kivuli wa Katiba, mwanzoni mwa mwezi huu, alidai bungeni kuwa Rais Magufuli amesababisha hofu ya kutumbua majipu kutanda nchi nzima, huku akimtuhumu kuwa ana viashiria vya udikteta.
Wanaomuombea
Wakati Makinda akiomba Watanzania wamuombee Rais Magufuli, huku viongozi wa Chadema wakipambana na hatua anazochukua dhidi ya wabadhirifu wa mali za umma, Askofu Mkuu wa Kanisa la Assemblies of God (TAG), jimbo la Kilimanjaro, Glorious Shoo, amesema uongozi wa Rais Magufuli, ni majibu ya maombi ya Kanisa na matarajio sahihi waliokuwa nayo Watanzania wote.
Askofu Shoo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, ambapo alisema kwa sasa heshima ya nchi imerudi baada ya mataifa mengine ya nje kujionea uongozi wa Rais Magufuli unavyopiga vita rushwa na dawa za kulevya.
Alisema kwa sasa Rais Magufuli, ameweza kurudisha ramani ya Tanzania iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kueleza kasi ya utumbuaji majipu inayoendelea ni jambo la kumshukuru Mungu, kwa kuipatia nchi kiongozi anayethubutu kuchukua hatua, bila woga kwa ajili ya kusaidia wanyonge.
Askofu Shoo alisema atashangazwa kuona kiongozi yeyote wa kisiasa atakayepinga yanayofanywa na Rais, kutokana na uwajibikaji na nidhamu mahala pa kazi kurudi.
Alipongeza hatua alizoita za kuponya fedha kwa kuwawajibisha watu waliosababisha upotevu wa fedha na kufanya mabadiliko yaliyochangia kuokolewa kwa fedha za umma, hali iliyosababisha heshima ya nchi kurudi katika mataifa mengine.
“Utendaji kazi na aina ya uongozi wa Rais Magufuli ni majibu ya maombi yetu sisi Kanisa na tunamuunga mkono kwa asilimia zote, kwani yale masuala makubwa na ya msingi ameyafanyia kazi bila woga wowote, ikiwepo vita dhidi ya rushwa, matumizi na biashara ya dawa za kulevya, uwajibikaji na nidhamu mahala pakazi, ni moja ya baadhi ya maeneo aliyoyagusa kwa muda mfupi na kuonesha matunda yake.
“Ukisafiri sasa sehemu mbalimbali za dunia, wanakueleza wanafahamu habari za Tanzania kama moja ya nchi inayopambana na rushwa kwa kasi kubwa pamoja na biashara ya dawa za kulevya, ambapo hapo awali Tanzania ilitajwa zaidi kwenye masuala ya kupitisha dawa za kulevya, lakini kwa kipindi hiki cha uongozi wa Awamu ya Tano hali imekuwa nzuri,” alisema Askofu Shoo.
Upinzani usipuuzwe
Alishauri viongozi wa upinzani wasipuuzwe licha ya baadhi yao kuwa na tabia ya kupinga vitu vinavyofanywa na Serikali, ambapo aliitaka Serikali kuchuja masuala ya msingi yanayosemwa na viongozi hao, ili yanayoweza kufanyiwa kazi kwa manufaa ya Watanzania wote katika kuiponya nchi, yafanyiwe kazi.
Alisema sasa ni muda wa kuweka siasa pembeni kwa vyama vyote, ili vishirikiane na Serikali iliyopo madarakani, ili mambo ya kweli yanayopigiwa kelele na upinzani kama yana ukweli yafanyiwe kazi na wananchi waridhike kweli yamefanyiwa kazi.
“Siasa ikae pembeni tuiponye nchi yetu wapinzani na Serikali kwa kumuunga mkono Rais Magufuli ...lakini tutaogopa kama kila jambo linalotoka kwa wapinzani litatupwa, tunatarajia baadhi yatafanyiwa kazi, pia wapinzani nao tutawashangaa sana wakipinga kila kinachofanyika na Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Askofu Shoo.
Alisema kwa sasa ni vyema Rais Magufuli aweke mfumo sahihi utakaokwenda na kasi yake, ili viongozi wengine watakaokuwa kwenye nafasi mbalimbali, wasitoke nje ya mfumo huo, ambao utazuia matatizo yasitokee.
Imeandikwa na Frank Leonard, Njombe na Arnold Swai,Hai.

No comments:

Post a Comment