Friday, 27 May 2016

JPM: Wazee wameharibu nchi

Imechapishwa gazeti la Mtanzania: Fri, May 27th, 2016


RAIS Dk. John Magufuli*Asema atabanana na wala rushwa kila kona
*Aeleza yuko tayari kuchunga ng’ombe kijiji
NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli  amesema wazee ndiyo wameharibu nchi hadi ilipofika sasa.
Amesema yuko tayari kurudi kijijini kwao akachunge ng’ombe kuliko kuwavumilia wala rushwa   nchini.
“Wazee tukitoka tuacha nchi safi, sisi wazee  ndiyo tumeharibu nchi hapa tulipofikia,”alisema Rais Dk. Magufuli
Rais alisema kutokana na uozo uliojaa serikalini, lazima ataendelea kuwachukulia hatua wanaokiuka taratibu za utumishi hadi   watendaji watakapobadilika.
Aliyasema hayo     alipofungua  mkutano wa Bodi ya Wakandarasi Tanzania, Dar es Salaam jana.
Alisema watendaji wa Serikali yake ni lazima wabadilike akisisitiza kuwa suala la utumbuaji majipu kwake siyo la muda mfupi na hatalibadili kamwe.
Kiongozi huyo wa nchi, alisema atahakikisha anaongeza vijana wengi katika  Serikali yake kwa sababu  hawapendi rushwa ingawa kuna watu wamekuwa wakiwachukia.
Alisema   atahakikisha   anajenga nidhamu ndani ya Serikali kwa kuwa na watumishi wenye kujituma kwa maslahi ya nchi na watu wake.
“Kazi hii  nilipewa na Mungu  sikupewa na mtu  yeyote, nipo  tayari kutoa sadaka mwili wangu kwa ajili ya watanzania wanyonge.
“Huo ndiyo mwongozo katika utendaji wangu  kamwe sitabadilisha, nitawashughulikia kweli kweli,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia changamoto ndani ya Serikali, alisema  pamoja na hali hiyo bado anafahamu umuhimu wa sekta ya ujenzi katika maendeleo.
Rais alisema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania   inapotangazwa zabuni za miradi ya ujenzi.
Lakini amewataka kujirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo serikali itaridhika.
“Nawatolea mfano… idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya, kwenye bajeti wana Sh bilioni 24.
“Makadirio ya kitaalamu yanaonyesha kila jengo lisizidi Sh milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwe kwa Sh bilioni moja  na Sh milioni 400!
“Sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo utapasua moyo. Hata kama utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa.
“Sasa mimi niwaombe ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi wazalendo, ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi,” alisema.
Rais aliwataka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa serikali   wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake watoe taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru)    watendaji hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za  sheria.
“Mimi niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa.
“Atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa huna hakika kama ile tenda utaipata.
“Wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa, mpaka anafilisika… kazi huipati na rushwa umeitoa,” alisema.
Vilevile, amewataka wakandarasi hao kujipanga ipasavyo  waweze kupata zabuni katika kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi   nchini ikiwamo ujenzi wa bomba la mafuta  kutoka Hoima  Uganda hadi bandari ya Tanga, ujenzi wa Reli ya Kati na ujenzi wa viwanda.
“Sina uhakika  mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata, ya kujenga bomba kutoka Hoima,   Uganda hadi Tanga.
“Nitasikitika sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania.
“Wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili.
“Tumejipanga kujenga reli ya kati ya Standard Gauge kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na kilometa 100.
“… lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China, tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 Standard Gauge, Central Corridor itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania mmejipangaje?” alisema na kuhoji Rais Magufuli.
Alisema kwa sasa   sekta ya kilimo  ambayo karibu ya watanzania asilimia 80 wanaitegemea huwezi ukawaacha wakandarasi  kwa sababu dhana wanazotumia  wengi  kwenye kilimo zimetengenezwa na wakandarasi.
Rais Dk. Magufuli alisema kuna sekta  nyingi zinategemea wakandarasi ikiwamo sekta ya uvuvi ambayo imekuwa ikichangia pato dogo kwa Taifa.
Alisema sekta ya madini  ambayo Tanzania imebahatika  kuwa na madini mengi,  karibu madini yote  yanayopatikana duniani,  na Tanzania yapo kwa asilimia kubwa.
“Madini hayo ambayo ni Tanzanite, Diamond Uranium na gram fight hadi gesi ambako tuna quebic feet  zaidi ya trilioni 59 za ujazo, kwa sasa zipo Tanzania.
“Vitu hivyo vinagusa wakandarasi  ukizungumzia suala la miundombinu  kwa sasa   kutakuwa na miradi  mikubwa katika nchi hii,”alisema Rais Dk.Magufuli.
Alisema imepangwa bajeti karibu asilimia 40 ambayo zaidi ya  trilioni 10 zitakwenda  kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 46 zitakwenda  kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilano.
RUSHWA
Rais Dk.Magufuli alisema   miradi hiyo inaweza kumalizika kwa  Sh milioni 200 ‘lakini unajua kabla hujamaliza lazima upeleke asilimia kwa mtu fulani’.
“Hiyo inaweza kuwa ni sababu  na kama hiyo ni sababu tuna chombo chetu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwa nini hamkitumii?  Kwa nini mnaungana na wale wanaomba rushwa?” alisema.
Alisema  kila mahali wanapokwenda kuomba zabuni wanaweka maslahi ya asilimia kwa ajili ya  kuchukua rushwa.
“Nimemleta hapa  Mkurugenzi wa Takukuru japo hakualikwa  kwa sababu ni mtu ninayemwamini.
“Inawezekana mnaowapelekea kesi nao ni wala rushwa. Huyu namwamini, kama kuna tatizo la rushwa  peleka taarifa   kwa Valentino,” alisema.
Akizungumzia madeni kwa wakandarasi, alisema  pamoja na kuwapo   tatizo la kuyalipa, Serikali itahakikisha inayalipa kwa wakati.
Kama ni tatizo la kulipa madeni yao sasa  limekwisha  na   Waziri wa Ujenzi, Uchuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amekwisha kulipa Sh bilioni 650, alisema.
Makombora
Rais Dk.Magufuli alisema changamoto kwa  wakandarasi  ni kutokuwa na ushirikiano na ubinafsi  ambao  ni ugonjwa  unaotakiwa kuombewa.
Alisema changamoto nyingine ni  wakandarasi  kutumia majina ambayo siyo yao.

No comments:

Post a Comment