Tuesday, 1 March 2016

Ukeketaji: Mila hatari ambayo bado inayosherehekewa TanzaniaKWA mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya wanawake na wasichana milioni 100 hadi milioni 140 duniani kote, wamefanyiwa ukeketaji ambapo kati yao milioni 92 wapo barani Afrika.
Ukeketaji unatajwa kuwa moja ya ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike na wanawake na pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu, ingawa ukatili huo unaendelea kufanyika na kusherehekewa na familia pamoja na jamii husika. Kwa mujibu wa WHO, matatizo mengi hutokea baada ya msichana au mwanamke kufanyiwa ukeketaji ikiwemo kutoka damu kupita kiasi, mshtuko, ugumu katika kupitisha mkojo, matatizo wakati wa kujifungua, maambukizi yakiwemo virusi vya Ukimwi na hata kifo.
Lingine lisilotajwa na WHO ni kwamba ukeketaji unachangia kuvunja ndoa kwa sababu katika jamii ya sasa yenye mchanganyiko mkubwa, mwanaume akifanya mapenzi na asiyekeketwa huona raha zaidi, hali ambayo inafanya ndioa za waliokeketwa kuwa hatarini. Tatizo lingine kwa wasichana waliokeketwa katika zama hizi, msichana huogopa kupata rafiki wa kiume asiye wa jamii yake na anapompata huwa na mashaka akichunga mwanaume huyo ‘asimguse’.
“Ukeketaji kwa wasichana na wanawake unaendelea kufanyika katika maeneo mengi bila kujali ni kosa la jinai kwa mujibu ya sheria ya kanuni ya adhabu,” maneno hayo yanasemwa na Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalopinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto (AFNET), Sarah Mwaga. Mwanga aliyasema hayo wakati akitoa tamko la Mtandao wa Mashirika yanayopinga ukeketaji Tanzania wakati wa siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji duniani inayofanyika kila Februari sita.
Kila Februari 6, Jumuiya ya kimataifa inaadhimisha siku ya kimataifa ya kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyodhalilisha utu na heshima ya mwanamke na msichana sehemu mbalimbali za dunia. Anasema jamii zinazofanyiwa vitendo hivyo zimeendelea kutafuta mbinu mpya ikiwemo kukeketa watoto wadogo mara wanapozaliwa. Mwaga anasema kwa takwimu za hivi karibuni takribani asilimia 15 ya watoto wa kike hukeketwa Tanzania ambapo takwimu hizo ni za kitaifa na kuna maeneo mengine ambapo asilimia hiyo iko juu kuliko ya kitaifa.
“Madhara ya ukeketaji ni makubwa na humwandama mwanamke katika maisha yake yote. Madhara mengine yanaonekana wazi, lakini mengine hujificha na kuibuka kidogo kidogo,” anasema. Anayataja madhara haya ni pamoja na kisaikolojia kutokana na maumivu makali ya kukatwa na kisu au wembe wa ngariba, kuuguza kidonda, maambukizi kwenye njia ya uzazi na ile ya haja ndogo, kupoteza damu nyingi na uwezekano wa kupoteza maisha, matatizo wakati wa kujifungua yakiongeza uwezekano wa kupata fistula, kuambukizwa VVU/ Ukimwi na pepo punda.
Akitoa mfano anasema kwa mkoa wa Mara, mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka wa ukeketaji kwa mujibu wa jamii ambazo zinadumisha mila hiyo ambapo wameshuhudia idadi kubwa kabisa ya watoto waliokeketwa pamoja na jitihada nyingi ambazo zimekuwa zikifanyika kukomesha vitendo hivyo. Katika wilaya ya Tarime ambayo ndio ina jamii zinazokeketa pamoja na Serengeti, takriban watoto 1,400 wamekeketwa na watoto hao ni kutoka katika koo za Bukira watoto 212, Bukenye watoto 230, Iregi watoto 800 na Nyabasi watoto 169.
Mkoani Mara, makabila ya Wajita wanaopatikana Musoma Vijijini, Bunda na Butiama pamoja na Wajaluo ambao wengi wao wako wilayani Tarime hawakeketi. Aidha katika Wilaya ya Serengeti walikeketwa zaidi ya wasichana 1,000. Pia katika mkoa wa Singida, hususani Wilaya ya Singida Vijijini, watoto hukeketwa wakiwa wachanga, hivyo inakuwa ni vigumu sana kupata takwimu za watoto waliokeketwa.
Kwa mujibu wa Mwaga, utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania katika shule moja Singida Vijijini mwaka 2015 ulionesha zaidi ya asilimia 80 ya watoto wa kike katika shule hiyo wamekeketwa lakini hawajui, kwani walifanyiwa hivyo wakiwa wachanga. Anasema wao kama wana mtandao wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ukiwemo utekelezaji wa sheria dhidi ya ukeketaji kugubikwa na vitendo vya rushwa, urasimu na sintofahamu kwa baadhi ya watendaji wa serikali, hivyo kufanya wale wanaovunja sheria kutochukuliwa hatua zozote au kesi kumalizwa nje ya utaratibu wa sheria.
Kadhalika kuna tatizo la wanasiasa kuogopa kukemea ukeketaji kwa hofu ya kunyimwa kura. Tatizo la urasimu katika sheria hiyo ya ukeketaji wakati mwingine imetajwa kwamba imechangia katika kuchelewesha au kupoteza haki kabisa. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema vitendo vya ukeketaji vinatakiwa kupigwa vita kila kona ili viweze kukomeshwa. Anasema kumekuwa na ongezeko kubwa la wasichana waliokeketwa.
Waziri huyo anasema katika mikoa ya Manyara kila watoto 100 basi 71 wamekeketwa, Dodoma kwa kila watoto 100, watoto 64 wamekeketwa, Arusha kwa kila watoto 100, watoto 59 wamekeketwa, mkoani Singida kila watoto 100, watoto 51 wamekeketwa na mkoani Mara kila watoto 100, watoto 40 wamekeketwa. “Hili ni janga ya kitaifa lazima kupambana nalo ambapo pia takwimu zinaonesha kuwa asilimia 15 ya wanawake hapa nchini wamekeketwa.”
Anasema ukubwa wa tatizo la ukeketaji katika mikoa hiyo linatokana na imani potofu na dhana hiyo imeanza kujitokeza katika mikoa mingine kama Dar es Salaam, Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila mbalimbali kuhamia mikoa hiyo.
“Serikali inapinga, inalaani na kukemea tabia ya kuendelezwa kwa vitendo hivi vya ukatili unaodhalilisha mtoto wa kike na mwanamke kwani unamsababishia madhara makubwa kiafya, kielimu, kisaikolojia na kimaendeleo. “Ndani ya serikali ya Rais John Magufuli tutamaliza vitendo vya ukeketaji. Natoa rai kwa jamii kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili mangariba na wakala wa mangariba waweze kujulikana na kuchukuliwa hatua,” anasema.
Waziri pia anawataka maofisa maendeleo ya jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwezesha kukamatwa kwa mangariba hao. “Maofisa ustawi wa jamii ambao vitendo hivyo vitatokea katika maeneo yao tutawachukulia hatua kuanzia sasa ni lazima washirikiane na viongozi wa kata, vijiji na hata mitaa ili kubaini vitendo hivyo.”
Aidha anasema serikali itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za hamasa na elimu kwa jamii zinazojikita katika kubadili fikra na mitazamo ya wananchi dhidi ya ukeketaji. Anabainisha kuwa pamoja na jitihada hizo bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwa kuwa suala la kubadili fikra na mitazamo ya jamii haliwezi kuisha kwa siku moja.
“Bado tunashuhudia vitendo vya kukeketa wasichana vikiendelea kutokea miongoni mwa jamii zetu, jambo hili linadhihirisha suala la kutokomeza ukatili wa kijinsia halitakwisha kwa kuitegemea serikali au sheria peke yake,” anasema. Pia serikali itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za hamasa na elimu kwa jamii zitakazojikita katika kubadili fikra na mitazamo ya wananchi dhidi ya ukeketaji. “Tutahakikisha sheria zinazomlinda mtoto wa kike na mwanamke zinafuatwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika na ukatili wa kijinsia,” anasema.
Mratibu wa programu za Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto, Cynthia Mushi alisema tatizo la ukeketaji lipo zaidi barani Afrika, hasa katika nchi za Burkina Faso, Benin, Niger na nchi nyinginezo ikiwemo Tanzania. Pia lengo la Umoja wa Mataifa kuanzisha siku hiyo ni kuhakikisha dunia inafikia ukeketaji sifuri ifikapo 2030.
“Inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 7.9 nchini Tanzania wamefanyiwa ukeketaji na hata ripoti ya afya na utafiti wa kaya ya Tanzania inakadiriwa ukeketaji kwa wasichana na wanawake wa kati ya miaka 15 hadi 49 ni asilimia 14.6 kwa mwaka na hiyo imepungua kidogo kwa asilimia 17.9 mwaka 1996. Anasema siku hiyo iliwekwa na Umoja wa mataifa Desemba 2012 ili kupiga marufuku mila na tamaduni zote zinazoendeleza vitendo vya ukeketaji. “Tatizo la ukeketaji lipo zaidi barani Afrika hasa kwa nchi kama Burkina Faso, Benin, Niger na nchi nyinginezo ikiwemo Tanzania,” anasema.
Mushi anasema lengo la Umoja wa Mataifa kuanzisha siku hiyo ni kuhakikisha dunia inafikia ukeketaji sifuri ifikapo mwaka 2030. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) mwaka 2014 zinaonesha zaidi ya wanawake na wasichana milioni 140 wanakeketwa kila mwaka duniani kote. Pia inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 7.9 nchini Tanzania wamefanyiwa ukeketaji kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa na Kuhudumia watoto (UNICEF, 2013).
Aidha kulingana na ripoti ya Afya na Utafiti wa Kaya ya Tanzania (TDHS) inakadiriwa kuwa ukeketaji kwa wasichana na wanawake wa kati ya miaka 15- 49 ni asilimia 14.6 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010. Hata hivyo, idadi hiyo imepungua kidogo kutoka asilimia 17.9 mwaka 1996 hali iliyochangiwa na kampeni ya uhamasishaji na uwepo sheria ya kanuni ya adhabu inayozuia vitendo hivyo kama sehemu ya vitendo vuya ukatili dhidi ya mtoto wa kike.
“Kwa kiwango kikubwa, vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikihusishwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mila na desturi, sheria za kibaguzi na utekelezaji duni wa sheria na sera,” anasema. Anasema CDF na wadau wanaopambana na ukeketaji wote kwa pamoja wanatambua jitihada zinazofanywa na serikali katika kupinga ukeketaji ikiwa ni pamoja na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa kama mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za mtoto wa mwaka 1989, mkataba wa kupinga aina zote za ukatili kwa wanawake wa mwaka 1979, mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Watoto ambayo Tanzania iliridhia mwaka 1991.
Pia Tanzania imeridhia baadhi ya mikataba na kuingiza kwenye sheria za Tanzania hususan kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya kanuni ya adhabu ya Tanzania ambayo inakataza ukeketaji kwa watoto. Anasema CDF kwa msaada wa UNFPA na wadau wengine wa maendeleo imeweza kufanikiwa katika kuwasaidia wasichana ambao tayari wameshaolewa, waliokeketwa na walioathirika na mimba za utotoni kwa kuanzisha na kusaidia vikundi, klabu za wasichana na wavulana ambazo pia hufanya utetezi kama njia ya kuzuia ukiukwaji wa haki za mtoto.
Aidha anasema wameanzisha vilabu 108 vya wasichana na wavulana vilivyopo nje na ndani ya shule zenye wasichana 1,952, wenye umri kati ya miaka 15-20 na mitandao mitatu yenye wanachama 30 kila moja. Mushi anasema wamefanikiwa kuwafikia watoto wa kike na wasichana 2,899 kupitia mafunzo, uhamasishaji na utetezi, kusaidia wasichana na wanawake wadogo 165 kuanzisha shughuli za kuwapatia kipato.
“Tumefikia zaidi ya watu 10,000 katika jamii kupitia kampeni mbalimbali na utetezi, tumefikia wadau wengine ambao ni walimu, Maofisa wa Wilaya na viongozi wa jadi 1,504,” anasema. Pia wamefanikiwa kufanya kazi kwa karibu sana na kituo cha masista wa Huruma Kiitwacho Masanga kilichopo wilayani Tarime ambao hutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na ushirikiano huo umeonesha mafanikio makubwa kutokana na ongezeko la wasichana wanaokimbia ukeketaji na kutafuta hifadhi kituoni hapo.
“Kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 kituo kimeweza kutoa hifadhi kwa jumla ya wasichana 2,126. Mwamako huo unaonesha jinsi wasichana walivyo na ari ya kukataa ukeketaji,” anasema. Mbali na mafanikio hayo anasema kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kukosekana kwa miundombinu na mifumo ya ulinzi ambayo inaweza kutoa ulinzi wa kutosha wa wasichana walio katika hatari na walioathirika na ukeketaji na mila zingine kandamizi.
“CDF inaitaka serikali kuwekeza katika raslimali zaidi na kuangalia mahitaji ya msichana ikiwa ni pamoja kuwa na mkakati na raslimali ambazo zitahakikisha maendeleo ya miundombinu ya ulinzi na vituo vya kutoa huduma kwa wasichana walio katika hatari kama vile waathirika wa vitendo viovu kupewa msaada wa kisaikolojia, kisheria na msaada wa matibabu,” anasema.