Tuesday, 1 March 2016

RIPOTI YA USAWA WA KIJINSIA DUNIANI - TANZANIA TUNARUDI NYUMA?

Ripoti mpya inayoonyesha usawa wa kijinsia duniani imetoka na nchi za Skandinavia bado zinaongoza (#1-Iceland, #2-Finland, #3-Norway, #4-Sweden). Kwa Afrika, Afrika Kusini (nafasi ya 6) na Lesotho (nafasi ya 10) ndizo nchi pekee za Kiafrika zilizomo katika kumi bora. Kwa Afrika Mashariki Uganda ndiyo inaongoza (nafasi ya 40), Tanzania imeshika nafasi ya 73 wakati Kenya ni ya 98. Marekani - ambako wanawake bado "wanabaguliwa" hasa katika suala la usawa wa mishahara, ajira, pamoja na mambo mengine - imeshika nafasi ya 31. Nchi ya mwisho ni Yemen (#134) ikifuatiwa na Chad (#133) na Pakistan (#132).

Baadhi ya vigezo muhimu vilivyozingatiwa katika uandaaji wa ripoti hii ni pamoja na usawa katika ushiriki wa shughuli za kiuchumi, usawa katika upatikanaji wa elimu ya viwango vyote, usawa katika upatikanaji wa huduma za afya na usawa katika ushiriki wa masuala ya kisiasa. Unaweza kuisoma ripoti kamili hapa na orodha ya nchi zote inapatikana hapa. Tovuti ya World Economic Forum ambayo huchapisha ripoti hii inapatikana hapa.

Jambo la kushangaza ni kwamba ripoti hii inaonyesha kwamba Tanzania inarudi nyuma katika juhudi zake za kuleta usawa wa kijinsia. Mwaka 2006 ilichukua nafasi ya 24, mwaka 2007 (nafasi ya 34), mwaka 2008 (nafasi ya 38) na mwaka huu (nafasi ya 73). Hii ni kweli?