Tuesday, 1 March 2016

CHOZI LA MWANAMKE! NAOMBA KUTOA HOJA


Naomba leo niweke ufafanuzi hapa wa kile nilichomaanisha katika makala yangu leo.
1.Kuzaa kwa shida:
Hivi ni nani asiyejua madhila wayapatayo wanawake sio tu wa vijijini hata wa mijini. Ni mara ngapi tunaoneshwa picha za wanawake waliojifungua katika Hospiali za mijini wakiwa wamelala wawili wawili kwenye kitanda na wengine wakiwa wamelazwa chini ya sakafu na vichanga vyao, huku vikipigwa na baridi. Huko vijijini napo kuna mengi yanasimuliwa, kuna idadi ya wanawake tena ya kutosha wanaojifungulia majumbani huku wakikosa huduma muhimu za kiafya, achilia mbali wale wanaojifungulia maporini kutokana na umbali mrefu kutoka nyumbani hadi vilipo vituo vya afya.
Sisimulii hadithi za alinacha hapa au hadithi za kufikirika, bali ninachokizungumza nina uhakika nacho na ninakifahamu kwa kuwa muda wangu mwingi nimekuwa nikiutumia vijijini hususana Arusha na Moshi.
2.Kulea kwa shida:
Hili la kulea kwa shida nalo halihitaji maelezao marefu, kwa kuwa kila kitu kiko wazi, kuna idadi ya kutosha ya wanawake wengi vijijini na hata mijini ambao aidha wametelekezwa na waume zao au wameolewa na wanaume amboa ni nusu wafu, yaani sio wazalishaji na badala yake huwaachia wanawake ndio wawe wazalishaji huku wakibeba majukumu mengine ya kifamilia, hebu tembelea kule feri au kwenye masoko ya mboga mboga kwa hapa jijini Dar, kuna idadi kubwa ya wanawake amboa huacha vitanda vyao aliajiri kuwahi feri kununua samaki au masokoni kununua mbogamboga na kuzichuuza. Huko vijijini napo naamini wengi mtakubaliana na mimi kuwa kuna mfumo dume ambao umetamalaki na wanawake wengi wa vijijini hawajui haki zao za msingi. Wanawake wengi wa vijijini hubeba majukumu ya kulea familia wenyewe huku wanaume wakijipa majukumu haba ambayo hayalingani na yale wanayoyabeba wake zao. Je hili nalo linahitaji ushahidi?
3.Kutafuta maji umbali wa kilomita kadhaa tena ya kisima:
kama kuna watu wanaotaabika na shida ya maji, basi ni wanawake na sio wa vijijini tu bali pia wa mijini, ukizungumzia shida ya maji, ni sawa na kuzungumzia madhila wayapatayo wanawake, kwa kule vijinini unaweza kukuta mke na mume wanatoka shamba na wakirudi nyumbani wakati mume anajipumzisha kivulini akipunga upepo, mke hakai chini anachukua ndoo ya maji na kwenda kutafuta maji umbali mrefu tu kwa ajili ya kuogea na kupikia. Kwa huku mijini napo, hata kama wote ni wahangaikaji kwa maan ya kutafuta mkate wa kila siku wa familia, lakini wakirudi nyumbani bado jukumu la kuteka maji linaachiwa mwanamke, niliwahi kukaa kwa mama yangu mdogo kwa muda kule kigogo., kama inavyojulikana kuwa kuna shida kubwa ya maji hasa katika maeneo mengi ya uswahilini katika jiji la Dar, nakumbuka siku hiyo tulikuwa umepanga foleni ili kuteka maji, ilikuwa ni folni ndefu ajabu, lakini cha kushangaza kila akija mwanaume na ndoo anapishwa ateke maji na kuondoka, nilipouliza niliambiwa kuwa wanaume hawapaswi kuweka foleni kwa kuwa wao eti ni watafutaji, kwa hyo wanaruhusiwa kuteka maji ili wakatafutie familia zao mkate wa kila siku. Ia walidai kuwa inawezekana mwanaume akawa anauguliwa na mkewe sasa ni vyema apewe nafasi ya kuteka maji ili awahi kumhudumia mgonjwa. Hizo ni busara za wakaazi wa Kigogo, lakini kwangu hilo halikuwa na mantiki, kwamba wanaume ni watafutaji na ndio sababu ya kupewa fursa ya kuteka maji bila ya kupanga foleni! Na wale wanawake ambo nao ndio watafutaji katika familia zao wanatambuliwa na kupewa nafasi hiyo? Je mnaona jinsi mfume dume unawavyowaingilia vichwani?
4.Kutafuta kuni umbali wa kilomita kadhaa:
Kutafuta kuni umbali mrefu, kama ilivyo katika kutafuta maji hili nalo ni shiranga jingine linalowaadhiri wanawake wa vijijini. Wengi tunafahamu ni kiasi gani wanawake wanataabika katika kutafuta kuni umbali mrefu. Hata watoto wa kike kule vijijini wengi hukwama kuendelea na masomo kutokana na kubebeshwa majukumu mengi ya nyumbani ukilinganisha na watoto wa kiume na hili la kutafuta kuni ni moja ya majukumu ambayo watoto wa kike hubebeshwa tofauti na wale wa kiume.
Kilio cha mwanamke wa Kiafrika ni nani akisikie!?:
Ninaposema kilio cha mwanamke, naangalia majukumu aliyobebeshwa mwanamke ukilinganisha na wanaume. Lakini pamoja na kubebeshwa majukumu yote hayo bado mwanamke huyu ameendelea kustahimili na kubeba majukumu hayo kwa unyenekevu mkubwa.
Kuna simulizi nyinge zinazohusu madhila wayapaayo wanawake katika vyombo vyetu vya habari kila uchao mpaka zimezoeleka masikioni mwa wanaume na ndio maana inaonekana kama vile wanawake ni walalamishi.
Naamini kuwa ufafanuzi huu wanawake watapewa nafasi na kuheshimiwa.