Dhana ya maendeleo iko kila mahali, katika maisha yetu binafsi, na katika maisha ya jamii na nchi kwa ujumla. Sote tunaamini kuwa tunahitaji maendeleo. Tusipofanya jitihada katika maendeleo, tunashinikizwa kwa namna moja au nyingine tufanye hiyo jitihada au tunaburuzwa tuendelee.
Katika kuziongelea nchi, watu hutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Kwa mujibu wa dhana hizo, nchi kama Marekani, Uingereza, Sweden, Ujerumani, na Japani zinahesabiwa kuwa zimeendelea. Lakini nchi kama Tanzania, Kenya, na Uganda zinahesabiwa kuwa nchi zinazoendelea. Dhana hizi zimejengeka vichwani mwa watu, tangu zamani. Je tunapotumia dhana hizi, tunaelewa tunachoongelea? Dhana hizi zina mantiki yoyote?
Binafsi, ingawa zamani nilikuwa na mawazo kama wengine, kwamba kuna jamii au nchi zilizoendelea na zile zisizoendelea au zinazoendelea, miaka hii nimegundua kuwa dhana hizi zina walakini au hazina mantiki bora. Nadiriki kusema kuwa dhana hizi zinadhihirisha kuwepo kwa kasumba vichwani mwetu, au elimu duni.
Kwa nini nasema hivi? Kwanza, kusema kuwa jamii fulani au nchi fulani imeendelea inaleta dhana ya kwamba jamii au nchi hiyo imefikia kilele na imegota hapo. Ukweli ni kuwa hakuna jamii wala nchi duniani ambayo imesimama tu. Kila jamii na kila nchi inabadilika muda wote, katika nyanja na vipengele mbali mbali: uchumi, siasa, utamaduni, na kadhalika. Hata hizo jamii au nchi ambazo zinasemwa zimeendelea nazo zinabadilika muda wote. Marekani ya mwaka juzi ni tofauti na Marekani ya leo, na Marekani ya miaka mitano ijayo itakuwa tofauti na hii ya leo. Kwa mfano, tekinolojia inabadilika muda wote katika nchi kama Marekani. Utamaduni na elimu ni hivyo hivyo. Na ndivyo ilivyo kwa nchi zote. Mabadiliko hayaishi, iwe ni katika Tanzania, Uingereza, au Marekani.
Kama huu mchakato na mabadiliko ndio maendeleo, basi kila nchi duniani ni nchi inayoendelea. Kwa hivi, dhana ya kuwepo kwa nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea haina mantiki bora. Ni upuuzi kuziweka baadhi ya nchi katika kundi la nchi zilizoendelea, wakati nazo ziko katika kubadilika muda wote.
Lakini, jambo la msingi zaidi ni kuitafakari dhana ya maendeleo. Tunapaswa kujiuliza: maendeleo ni nini, na nani anayeweka vigezo vya kupima haya maendeleo? Hili ni suali la msingi.
Kwa ujumla, baadhi ya nchi, hasa zile zilizotutawala wakati wa ukoloni, na zile zenye nguvu katika dunia ya leo, ndizo zinazoweka vigezo vya maendeleo. Kwa vile Ulaya inajitapa kwamba imeendelea, Waafrika na wengine sehemu mbali mbali za dunia nao wanakubali hivyo na kuziona nchi zao kuwa ni nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Hayo ni mawazo ya kikoloni mamboleo. Ni kasumba ambayo ilienezwa na inaendelea kuenezwa mashuleni, katika vyombo vya habari, na taasisi nyingine nyingi.
Tunao wajibu wa kujikomboa kimawazo ili tuweze kufikiri sisi wenyewe, badala ya kuwa kasuku. Tuwe na vichwa timamu vya kutuwezesha kuyatafakari masuala sisi wenyewe. Tunapaswa tujijengee huu msingi ili tuweze kuitathmini dhana ya maendeleo, tuweze kujiuliza maendeleo ni nini? Katika kufanya hivyo, tuweze kujiuliza iwapo dhana ya maendeleo iliyoko Ulaya ni sherti tuipokee na kuikubali. Katika kutathimini suala la maendeleo, tunapaswa kuchukua jukumu na wajibu wa kujitungia vigezo vyetu na kuvitumia. Lazima tujenge utashi wa kujiamini na kujiamulia mambo yetu wenyewe kwa manufaa yetu.
Bila kufanya hivyo, tutabaki kuwa kasuku. Chochote wanachofanya Ulaya au Marekani, chochote kilichopo Ulaya au Marekani, au chochote kinachotoka huko tunakiona ni maendeleo. Tunaamini kabisa kuwa kuwaiga watu wa Ulaya na Marekani ndio maendeleo. Wao wakianzisha kitu, nasi tunataka tufuate. Vigezo vya elimu, utawala bora, demokrasia, na kadhalika vinawekwa na wao. Sisi tumekuwa watu wa kufuata.
Papo hapo, watu wa Ulaya na Marekani hawaoni mambo yetu kuwa ni maendeleo. Ni pale tu tunapoiga mambo yao ndipo tunahesabiwa kuwa tunaendelea. Hata tukaanzisha jambo, hawaoni kuwa ni maendeleo. Na sisi wenyewe, kwa kuangalia Ulaya na Marekani, hatuamini kuwa tunachofanya ni maendeleo. Kitu hichi kingeanzia Ulaya au Marekani, tungekiona kuwa maendeleo.
Hata kama jambo halina maana, au lina madhara, maadam linatoka Ulaya au Marekani, watu katika nchi zetu wanaliona ni maendeleo. Hata kama ni mambo yasiyoendana na utu, maadam yametoka Ulaya, watu wetu wanayaona ni maendeleo.
Naweza kutoa mfano moja. Nchi zinazoitwa zimeendelea zimefanikiwa kujenga miji mikubwa, viwanda, na miundombinu ya aina aina, na hivi kuonekana zimeendelea. Pamoja na kuwa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika haya maendeleo, dhana ya kuwa hizo ni nchi zilizoendelea inabaki pale pale, na sisi tunakazana kuiga waliyofanya wao. Tunahangaika kufuata mkondo ule ule na kuharibu mazingira kwa ujenzi wa viwanda na miundombinu mbali mbali. Hatujali kuwa haya yanayoitwa maendeleo yameharibu na yanazidi kuhatarisha mazingira. Tunataka viwanda, bila kuangalia athari zake katika maji tunayotumia, hewa tunayovuta, na mazingira kwa ujumla. Hatujali kuwa maendeleo ya Ulaya na Marekani yameharibu mahusiano ya jamii. Je, hayo ndio maendeleo?
Kama nilivyosema, hakuna nchi ambayo imesimama tu na haibadiliki. Kosa tunalofanya ni kutozingtia ukweli huo na badala yake kuziona nchi za Ulaya na Marekani kama nchi zilizoendelea. Kwa mtindo tulio nao, wa kufuata kila kinachotoka Ulaya na Marekani, tutabaki na hii dhana ya kujidunisha, ya kujiona sisi ndio nchi zinazoendelea au zisizoendelea.
Kwa mtazamo wetu huu, hatutafikia kuwa sambamba na nchi hizo tunazosema zimeendelea. Tutabaki tukiamini kuwa sisi ni nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Watu wa Ulaya na Marekani wataendelea kuyaona yale wanayofanya kuwa ndio maendeleo, na wataendelea kutushinikiza katika njia wanayoona wao kuwa ya maendeleo. Sisi tutakuwa daima watu wa kufuata. Kuna mipango mingi katika nchi yetu, ambayo inaitwa mipango ya maendeleo, inayofuata msingi huu na kuna taasisi nyingi kutoka nje ambazo zinafanya shughuli hizo zinazoitwa za maendeleo katika nchi yetu. Kwa mtindo huu wa kujidhania tuko nyuma, tutabaki nyuma daima.
Tunawajibika kujikomboa kifikra, tuweze kujiwekea vigezo vyetu wenyewe. Pasipo kuwa na vigezo vinavyozingatia haki ya kila watu duniani kuchangia katika kutunga tafsiri na viwango vya maendeleo, si sahihi kuendelea kutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Inatubidi tubadili fikra; tukatae huu mkondo uliopo sasa wa kuitwa au kujiita nchi zinazoendelea. Ni fikra tegemezi, za kikasuku, na kikoloni mamboleo. Athari za hizi fikra tegemezi zinaonekana kila mahali.
Tunapoongelea mfumo wa uchumi, kwa mfano, tunajikuta tunahangaika kuiga mambo ya Ulaya au Marekani. Tunapoongelea elimu, ni hivyo hivyo. Tunahangaika kufuata viwango vya Ulaya au Marekani. Leo hii, mtu akianzisha shule na kuiita Cambridge Academy halafu mwingine aanzishe yake na kuiita Upogoro Academy, watu watavutiwa zaidi na Cambridge Academy, bila kutafakari. Tunapoongelea urembo, kwa mfano, ni hivyo hivyo. Vigezo tunaiga vya Ulaya na Marekani.
Kutokana na fikra zetu hizi, mitumba kutoka Ulaya na Marekani tunaiheshimu sana. Vyakula kutoka huko navyo tunavienzi sana, hata kama havina ubora kiafya. Watu wa Ulaya na Marekani wakija kwetu na kujinadi kama wataalam tunawashabikia sana, hata kama watu hao ni mbumbumbu. Kwa vile tunaamini Ulaya na Marekani wameendelea, hatuwazii kuwa kuna mbumbumbu huko. Lakini mtu kama mimi, ambaye nimefundisha sana huko Marekani, ninajua kuwa Marekani, kama ilivyo Tanzania, kuna wenye vichwa na mbumbumbu pia wako.
Kuhitimisha, turudi kwenye suali la awali: maendeleo ni nini? Maendeleo ni mabadiliko katika kitu au hali yoyote, katika nyanja mbali mbali za maisha, mabadiliko ya manufaa kwa mujibu wa mazingira husika. Katika jamii au nchi, maendeleo yanaboresha maisha ya binadamu, yanahifadhi au kuboresha mazingira, na yanaendana na heshima, utu, na haki. Maendeleo yanatokana na msukumo wa jamii au nchi husika, kwa mujibu wa mahitaji yake halisi, na kwa mujibu wa maamuzi na matakwa ya jamii hiyo, maamuzi yatokanayo na fikra huru na tambuzi, zenye mwelekeo wa ukombozi. Maendeleo hayaathiri mazingira bali yanadumisha muafaka na kuyaboresha. Maendeleo hayaleti matabaka miongoni mwa wanadamu. Kama kuna kuiga, uigaji huo unazingatia vigezo hivyo vyote, na umejengeka katika kuheshimiana, si kushinikizana.
No comments:
Post a Comment