JITIHADA za kutosha zinahitajika katika jamii ili kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinakomeshwa badala ya kuwaachia jukumu hilo wanasiasa pekee na baadhi ya makundi katika Jamii.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali zilizowahi kutolewa katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwapo na mmomonyoko mkubwa wa maadili nchini, jambo ambalo linachangia kasi kubwa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika sehemu zote za Tanzania kwa maana ya Bara na Visiwani.
Matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekuwa yakiwaathiri wanawake na watoto nchini yahahusu ubakaji, ulawiti, vipigo kwa wanawake, tohara za wanawake na wasichana, ndoa za utotoni na mimba za utotoni.
Nyingine ni kuwanyima fursa za elimu watoto wa kike, kuwazuia wanawake kurithi mali, mirathi, talaka, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wanaume kutelekeza familia.
Kwa miaka mingi sasa, wanawake wamekuwa wakiiomba Serikali kupigania haki zao kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuwachukulia hatua za kisheria wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia tokana na matukio hayo kukithiri katika jamii.
Jamii inashuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiongezeka siku hadi siku huku kundi linaloathirika zaidi ikiwa ni watoto na wanawake.
Imefika wakati sasa jamii isichoke kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia. Vilevile, maonyesho ya programu mbalimbali za asasi zinazolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia na kutoa mada mbalimbali zinazohusiana na ukatili huo ni muhimu ili kutokomeza kabisa tatizo hilo.
Aidha, jamii nzima inatakiwa kuelimishwa kwamba athari dhidi ya mwanamke ni kitendo hasi kutokana na mwanamke kuwa tegemeo kubwa katika jamii na zaidi katika ngazi ya familia.
Uchunguzi wa SMGEO katika maeneo tofauti nchini na Visiwani, umebaini kuwa tatizo la udhalilishaji wa kijinsia, kwa kiasi kikubwa umepelekea waliotendewa ukatili kupata matatizo ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kukwazwa kimaendeleo na kukosa sehemu ya kuelekea.
Katika uchunguzi huo, imebainika kwamba hatua ya mijadala iliyowahi kushika kasina kuibua mijadala mizito nchini, imechangia kutoa mwanga kwa wananchi wengi na kuibua vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wote wanapokutana na matatizo kama hayo inagawa baadhi yao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kudhalilisa wanawake na watoto.
Hata hivyo, jinsi vyombo vya habari vinavyoripoti matukio hayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuangaliwa kwa pande zote za Shilingi ili kuwasikiliza walalamikaji na walalamikiwa kwa kuwa hizo ni tuhuma ambazo zinahitajika kufanyiwa maamuzi na Mahakama.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na timu ya waandishi wetu Jijini Dar es Salaam, walisema Serikali zote ziweze kusikiliza kilio cha jamii kuhusiana na kasi kubwa ya matukio ya ukatili na kuchukua hatua kwa kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Sophia Gipson, amesema katika kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa katika jamii, kuna umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwa kuwaweka wazi wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Bado kuna wanawake na wasichana ambao wanaamini wameumbwa kwa ajili ya kufanya shughuli za nyumbani pamoja na kumhudumia mume na watoto na ndiyo hao ambao wanashindwa hata kutoa taarifa kuhusiana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa”alieleza Sophia.
Katika hatua nyingine Serikali imetakiwa kupitia upya na kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaonekana kutoa mwanya kwa wazazi kuwaozesha mabinti zao kuanzia umri wa miaka 14.
Bila shaka maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na maadamano makubwa ambayo yatakuwa yanaratibiwa na mashirika mbalimbali ya wanaharakati nchini ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili dhidi ya kijinsia hususani kwa watoto na wanawake.
Katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya mashirika yakiwemo, Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLADF), Mtanadao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika la jinsia (SMGEO)Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Chama cha Wanasheria wa Tanzania (Tawla), Chama cha Wanasheria Zanzibar (Zafela), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mengine yamekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili na ni miongoni mwa wanaoratibu maandamano hayo.
No comments:
Post a Comment