Monday, 3 July 2017

Tumuunge mkono mh. Rais kupinga mimba mashuleni !!!

*Na Mwalimu Upendo Chikoti* Tangu Mhe. *Rais JOHN POMBE MAGUFULI* alipotoa kauli yake ya kutopokelewa kwa wanafunzi wanaotoka kujifungua katika shule za umma, kauli hiyo imeibua mijadala mbalimbali katika jamii, huku walio wengi hususani wanaharakati wakionekana kumpinga kwa madai kuwa hatua hiyo ya Mhe. Rais ni ukiukaji wa haki za elimu kwa watoto wa kike.
Ukweli ni kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajali, inalinda na kutetea haki na ustawi wa watoto wa jinsia zote kwa kusimamia sheria, sera na mikataba ya Kimataifa inayolinda haki na ustawi wa mtoto. Kwa kulitambua hilo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu. Kwa Mfano, utekelezaji wa Mpango wa Elimu kwa Wote (Universal Primary Education-UPE), Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), Mpango Maalum wa Elimu kwa Walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) na sasa Mpango wa Elimu Bure kwa shule ya Msingi na Sekondari. Lengo la hayo yote ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote (wakiwemo watoto) wanapata Elimu kama haki yao ya msingi. Hata hivyo, bado jamii imekuwa ikichangia kukwamisha jitihada hizo kwa kuzuia watoto wao kwenda shule kwa kuwatwisha majukumu mbalimbali kama vile kazi za ndani, kuchunga mifugo, kilimo, biashara, huku wazazi na walezi wengine wakidiriki kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa ili wasiendelee na masomo na kupata nafasi ya kuwaozesha katika umri mdogo. Hivyo tusitumie kauli ya Mhe. Rais kama chanzo cha ukiukaji wa haki za watoto kwani ukiukaji wa haki za watoto unafanywa na jamii yenyewe kwa kushindwa kutimiza wajibu wake wa kumlea mtoto katika maadili, mila na desturi za Kiafrika na badala yake tunatumia Mikataba ya Kimataifa kuharibu tamaduni, mila na desturi zetu. Yatubidi tutambue kuwa mikataba hiyo inapaswa kutekelezwa bila kuathiri mila, tamaduni na desturi zetu. Aidha, Serikali imekuwa ikipinga mambo yote ambayo yana athari katika jamii licha ya kwamba yana sura ya haki za binadamu katika jamii husika na ndiyo maana imekuwa ikipinga vikali suala la mapenzi ya jinsia moja, ukeketaji na mengine mengi kutokana na athari zake kwa jamii. Aidha, kwa mujibu wa mafundisho ya Dini na tamaduni za Kitanzania ni dhambi na mwiko kwa mtoto kushiriki tendo la ndoa kabla ya kuolewa. Hata katika nchi za wenzetu hasa Uarabuni ni marufuku mwanamke kuzaa nje ya ndoa. Je kuhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo siyo kwenda kinyume na mafundisho ya dini? Tusijikite zaidi kupigia kelele suala la wanafunzi hao kurudi shuleni baada ya kujifungua, bali tufikirie pia athari zinzoweza kumpata wakati wa kujifungua, malezi ya mtoto atakayezaliwa bila kusahau kuwa mtoto huyo naye anahitaji kutimiziwa haki zake za msingi. Je watatengewa vyumba vya kunyonyeshea mashuleni? Wakiugua nani atawahudumia? Ni dhahiri kuwa hatuwezi kupinga mimba za utotoni, ndoa za utotoni, watoto wa mitaani, ombaomba wala kumaliza tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi katika umri mdogo kwa kubariki mimba mashuleni. Ni ukweli usiofichika kuwa wanafunzi walio wengi wamekuwa wakipata ujauzito kwa kurubuniwa na watu wao wa karibu kwa vitu vidogo kama fedha, chips, vizawadi na starehe binafsi. Watu hao tunaishi nao katika jamii zetu na hata baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakishiriki kuwalinda ili wasifikiwe na mkono wa sheria. Ni vema tukatambua kuwa tamko la Rais ni Sheria kwa mujibu wa katiba ya nchi. Hivyo ipo haja sasa kila Mtanzania kwa nafasi na wadhifa alionao kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kuelekeza nguvu zaidi katika elimu rika kwa watoto na kuelimisha jamii juu ya athari za mimba za utotoni na umuhimu wa kulinda haki za watoto na kuwafichua wale wote wanaokwamisha watoto kutimiza ndoto zao ili sheria ichukue mkondo wake. Mwalimu Upendo Chikoti Shule ya Msingi Mkonze - Dodoma