Friday, 4 March 2016

NAFASI YA MWANAMKE NA MAMA KATIKA MAISHA YA FAMILIA

Tuchambue kwa mapana na kina wajibu wa Familia katika Ulimwengu mamboleo; Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wa Mungu alimuumba. Alimuumba Mwanaume na Mwanamke......katika maana hiyo, wote wana usawa halisi katika sura ya Mungu. Hakuna aliye zaidi ya mwingine, lakini anawaumba kama Mwanaume na Mwanamke hivyo mahusiano yao wawili ni ya Mke na Mume. wanapojaliwa zawadi ya watoto basi huyu Mke anakuwa Mama yao. Na hii ndiyo maana tunasema huyo ni Mama na Mwanamke wakati huo huo.

Waraka wetu huu unaitaka Jamii itambue usawa wa Wanawake katika ugawaji wa majukumu....Mwanaume asipendelewe na Mwanamke akatupwa nje kama ambavyo historia inaonyesha kwa wakati uliopita. Lakini pia tunaitaka Jamii inapogawanya majukumu ihakikishe kwamba Mama asije akapewa majukumu yanayomtenga sana na Familia, kwani Umama wake ni wa lazima sana katika makuzi ya watoto kiasi kwamba hakuna mwingine zaidi ya Mama.

Waraka huu unaonya kwa ukali kabisa kuhusu tabia ya ukandamizaji na unyanyasaji wa Wanawake unaofanya waonekane kama watumwa katika kila nyanja ya maisha kama; katika elimu, ajara na mishahara.


Ukweli usiopingika kuwa kwetu Afrika Jamii nyingi zinampa Mwanamke nafasi ya mwisho na kwa udhaifu huu hata ndoa za wake wengi zinakubalika tu! Tumshukuru Mungu kuwa leo kwa jitihada mbalimbali za Serikali nafasi sawa kwa wote inasisitizwa na jitihada mbalimbali zinafanyika kila mahali kumwinua Mwanamke kwa kupitia Vikundi vya umoja wa Wanawake. Tuendelee kuunga mkono jitihada hizi katika Jumuiya zetu, Makanisani mwetu, Misikitini, Majimboni mwetu na Nchini mwetu na kokote tunapofanya kazi. Katika jitihada hizi ni vizuri pia kuwa macho....kuwa Mwanamke na Umama ni hadhi kubwa sana ambayo hatupaswi kuiacha na kutafuta kuwa kama Mwanaume au Baba wa familia. Ni vizuri kila Mwanamke ajivunia; Umama wake, aupende, auheshimu na kuutunza kama alivyofanya Bikira Maria, kiasi cha kuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno la Mungu aliyefanyika Mwili akakaa kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Wanawake wasikubali kamwe kuwa ni Vichokoo vya matangazo ya biashara, watambue na kuthamini Utu na Heshima yao katika mpango mzima wa kazi ya uumbaji.

No comments:

Post a Comment