Friday, 4 March 2016

EPUKA TABIA YA UKALI, UKAIDI NA UGOMVILeo tutaona kanuni au mbinu nyingine za kuishi na watu vizuri ukiwa ni mwendelezo wa pale ilipoishia.
Jifunze kuomba msamaha kwa Mungu. Ni vizuri kuomba msamaha mbele ya Mungu wako aliyekuumba.
Vile vile wakati mwingine unaweza kumkosea mzazi wako, ndugu yako, rafiki yako na majirani zako, hivyo ni vizuri kujutia makosa yako ukimuomba Muumba wako pamoja na yule uliyemkosea wakusamehe.
Heshimu, fikira, mawazo na maoni ya wengine. Ni vizuri kuheshimu maoni ya wengine wakati mnapokuwa kwenye kikao, mjadala au majumuisho ya mambo mbalimbali yaliyotokea.
Kumbuka unapokuwa mtu wa kuheshimu fikira, mawazo na maoni ya wengine hata wewe mwenyewe utapata heshima.
Hali hiyo itampa mtoa maoni ujasiri wa kujieleza vizuri na kwa uwazi pasipo hofu.
Jifunze kuzuia misisimko ya mwili kama vile hasira, tamaa za mwili, kucheka au kufurahi kupita kiasi.
Wote tunajua kuwa misisimko ya mwili inatokea pale mtu anapopata hisia ya jambo fulani.
Kama ni msiba tunajua unaleta simanzi moyoni, harusi inaleta furaha na unapokasirishwa inaleta hasira.
Hivyo basi, mara nyingine ni vema kujizuia pasipo kuonyesha hisia hizo katika baadhi ya maeneo ambayo unajua hisia yako itachukuliwa katika hali tofauti.
Kwa mfano, imetokea rafiki yako wa karibu akawa amekuahidi kukupatia fedha ulizomuomba siku fulani, lakini kwa bahati mbaya akawa hakufanya kama alivyokuahidi.

Jambo hilo linaumiza, hivyo ni vizuri kuficha hasira yako kwani wakati mwingine inaweza ikakufanya mkosane na rafiki yako au ukapatwa na vidonda vya tumbo pasipo kujijua kwa sababu ya hasira.
Au wakati mwingine unaishi na familia yako hivyo labda wewe ni kijana wa kiume unakuwa na rafiki wako wa kike, kutokana na mahusiano yenu ya karibu mnajikuta mnashindwa kujizuia misisimko yenu na kuionyesha mbele ya familia yako, jambo linaloweza kukuletea matatizo aidha kwa mpenzi wako kuchukiwa na familia au kukataliwa na familia yako. Jambo kama hili litaleta dosari kwako wewe na uliyempenda, ikizingatiwa kuwa wote ni wa muhimu kwako.
Hivyo basi, jitahidi kujijengea heshima katika suala kama hilo ili lisikuharibie.
Ni vizuri kujenga hali ya kujithamini na kujiamini. Penda kujenga tabia ya kujithamini na kujiamini. Hali hii itakupa ujasiri.
Ni vizuri kuyathamini maisha yako kwa upande wa malazi, mavazi na chakula. Pia unapojiamini katika mambo mbalimbali itakupa ujasiri wa kutokukata tamaa katika jambo lolote.
Kwa mfano, wewe ni mwanafunzi na umejijengea tabia ya kujiamini kuwa unasoma kwa bidii ili ufaulu. Basi kujiamini huko kunaweza kukuongezea motisha ya kufanya vizuri katika masomo yako, tofauti na mwanafunzi yule anayejiona hawezi hata akisoma haelewi.
Au kwa mwanachuo aliyemaliza masomo yake na aliyekuwa akitafuta ajira bila mafanikio, lakini amekuwa akijiamini kuwa kutokana na vyeti vyake vizuri alivyo navyo ipo siku atafanikiwa. Unakuta kuwa hata kama itachukua muda mrefu kutokana na kujiamini ipo siku atafanikiwa na kupata ajira.
Epukana na tabia ya ukali, ukaidi na ugomvi. Ili uishi na watu vizuri epuka tabia ya ukali usiokuwa na maana.
Ukali usiokuwa na maana ni ile tabia ya kufokafoka ovyo, hali inayofanya udharauliwe hata na watoto wadogo.
Mfano mzuri ni mashuleni. Utakuta baadhi ya walimu wakali kila wanapoingia darasani wanafunzi wengi wanadharau kumsikiliza matokeo yake wanafeli.
Matokeo yake hasara inakuwa ni kwa mwanafunzi na mwalimu anaonekana kuwa hajui kufundisha. Hivyo ukali haujengi bali unaharibu.
Tabia ya ukaidi au ujeuri na ugomvi ni tabia mbaya katika jamii. Jifunze kuishi na watu pasipo malumbano wala magomvi.
Unapokuwa na tabia ya ugomvi wa mara kwa mara unajishushia hadhi yako kwa kuwa kila mara utataka malumbano hata kwa jambo dogo. Jiheshimu uheshimike.
Kunapotokea kutoelewana tafuta njia ya kumaliza matatizo, wala usiwe na kinyongo. Mara nyingine inaweza ikatokea hali ya kutokuelewana kati ya mume na mke, baba na watoto au mama na watoto, bosi na wafanyakazi wake au majirani kwa majirani.
Hali hii inapotokea jitahidi kutafuta njia muafaka ya kutatua tatizo hilo ili lisiwe kubwa hata kusababisha athari kubwa zaidi.
Hili likifanikiwa kutakuwa na mahusiano mazuri nyumbani kwako, kazini, shuleni na hata na jirani yako. Penda kuwa msuluhishi wa mambo kunapotokea matatizo.
Jifunze kusamehe na kusahau, kwani watu wote wanakosea. Ni mtihani mkubwa kwa watu wengi kuhusiana na hali ya kusamehe na kusahau anapokosewa na mtu, lakini katika vitabu vyote vya dini vinasisitiza kuhusu kusameheana.
Epuka tabia ya kulipiza kisasi. Tabia hiyo si nzuri, kwani mwenye tabia kama hiyo anapotukanwa na yeye hutukana, anapopigwa naye hurudisha au anaponyimwa kitu chochote anachohitaji kutoka na jamaa yake naye hulipiza hivyo hivyo.
Epukana na tabia ya kujitenga na wengine. Katika kanuni za kuishi na watu tabia hii si nzuri. Ni vizuri ukawa mtu wa kuchanganyika na jamii katika makundi mbalimbali. Pia epukana na tabia ya kushurutisha, unapotaka kitu au kutoa amri unapotaka kitu kitendeke.
Kuna watu wengine ndivyo walivyo yaani hujiendekeza kung’ang’ania tabia zisizostahili za kutaka kushurutisha wengine wafanye kitu fulani ilhali yeye hakifanyi…ndivyo alivyojilea.
Sikubaliani na watu wanaosema ndivyo alivyozaliwa kwani hiyo tabia inaepukika.
Watu kama hao hupenda kutoa amri na kuwashurutisha wengine kufanya jambo ambalo yeye hapendi kulifanya ili mradi tu aonekana kuwa na yeye ana sauti katika jamii.
Ni vizuri kueleza jambo kwa ustaarabu kila unapotaka kitu na si kuamrisha.Epukana na biashara au na shughuli zisizo na uhalali. Unapofanya shughuli au biashara isiyo halali inakuondolea uaminifu kwa jamii inayokuzunguka.
Kwa mfano, mtaani kazini kwako unakuwa mtu usiyeeleweka kwa kuwa watu wanakuwa wakijiuliza unafanya shughuli gani bila majibu.
Vile vile biashara hizo zinaweza kukusababishia matatizo kama ya kufunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani endapo utakutwa na kosa.
Jifunze kutokuwa mchoyo au uwatakie watu wengine mambo mabaya. Baadhi ya watu waliofanikiwa huwa hawapendi maendeleo ya wengine.
Wanapoombwa msaada ni wagumu kutoa. Mfano, kwa baadhi ya wanafunzi mashuleni ambao wamejaaliwa akili huwa hawapendi kutoa msaada kwa wenzao. Hata maofisini kuna baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya wenzao kwa kumsemea mambo yasiyo ya kweli kwa mabosi wao.
Epukana na lugha ya ubinafsi, mimi, changu, tumia chetu na sisi. Lugha hizo si nzuri katika jamii inayokuzunguka. Unapokuwa na tabia hiyo inakujengea chuki miongoni mwa wanaokuzunguka.
Ni vizuri kushirikiana vifaa vya ofisini, shuleni na katika maeneo mbalimbali na jamii.Inawezekana wakati mwingine mtu anakuwa na lugha hiyo ya ubinafsi, ‘mimi, changu, chetu na sisi’ kutokana na mazingira yaliyopo ya sasa.
Mfano yeye ni msafi na wenzake anaoishi nao kufanya kazi nao au kusoma nao wanakuwa na tabia ya uchafu na ameshajaribu kuwabadilisha bila mafanikio, ni vizuri kutumia busara ya kuwaelimisha zaidi.
Hii itakusaidia kila mtu kutumia kifaa chake mfano vikombe maofisini kila mtu ana usafi wake, vioo kwa akina dada, vitana vya kuchania nywele na mfano wa vitu kama hivyo. Jitahidi kutokuonyesha hali hiyo kwa gharama yoyote ile.
Unapomsaidia mtu usifanye hivyo kana kwamba umemnunua. Watu wengine wanapotoa msaada kwa wenzao hujisahau na kuanza kutangaza au kumnyanyapaa yule aliyemsaidia huku akiona ni sawa.
Mfano rahisi unakuta labda kuna watu wengine wamewapokea ndugu zao au watu wasio na uwezo na kuishi nao nyumbani kwao.
Kutokana na kuishi nao basi ufadhili unageuka kuwa mateso kwa kuwa kila kazi ataifanya huyo aliyesaidiwa au kila mara atakuwa anatumwa maeneo ya mbali mara nyingine pasipo hata na nauli.
Si vibaya kumtuma wala si vibaya kusaidiwa na mtu kama huyo, ila isivuke mipaka itakujengea picha mbaya kwa wanaokufahamu pamoja na huyo unayemsaidia atakapoamua kuondoka kwako.
Epukana na tabia ya kugombeza, kutukana au kudharau wengine. Watu wengine wamejiendekeza katika tabia ya kupenda kugombagomba ovyo bila sababu, kutukana au kudharau wengine.
Hii ipo sana maofisini kwa mabosi walio wengi hujisahau kuwa nafasi wanazokalia ni za muda tu, hivyo hudharau wale walio chini yake kwa kuwasema sema ovyo na kuwatukana pasipo sababu ya msingi.
Hata kwa upande wa baadhi ya wanawake na wanaume wawapo nyumbani, huwa na tabia hiyo kwa watoto wao na hata wafanyakazi waliowaajiri au ndugu wanaoishi nao.
Ni vizuri kuacha tabia hiyo mara moja kwani inakuondolea heshima na kukufanya udharaulike.
Pia wakati mwingine utakuta wenye mali si wasemaji lakini wale wanaowaachia majukumu kidogo ndiyo wanaokuwa na tabia hizo mbaya katika jamii.
Gombeza pale inapostahili lakini isiwe mazoea, kamwe usitukane wala kuleta dharau kwa wengine, huo ni utovu wa nidhamu.
Jifunze kuvumilia mienendo ya imani ya dini nyingine. Suala hili katika jamii yetu inayotuzunguka limekuwa likileta mizozano na wakati mwingine watu huamua kupigana.
Mnapokuwa watu wenye imani za dini tofauti katika ofisi zenu, vyuoni au hata kwenye mikusanyiko mbalimbali, jaribuni kuvumilia kila hatua ambayo kwako unaiona ni kinyume na maadili yako. Ukishindwa hali hiyo ni vizuri uondoke na kuwapisha wenyewe waendelee.
Mfano kwenye msiba labda wewe ni wa madhehebu fulani hivyo umeenda kwenye msiba wa imani tofauti na yako, ni vizuri kufuata taratibu zao, kama unajiona huwezi basi ili kuepusha shari ondoka eneo hilo uwaachie wenyewe ili usionekane kituko.
Ni vizuri ukae kimya uwaachie wenyewe waendelee na ratiba na shughuli zao kuliko kuanza kupayuka ovyo au kukosoa katika msiba huo