Thursday, 10 March 2016

Je, kuna usawa Afrika Mashariki? Au la? Utajiri, umaskini na usawa ndani ya Kenya, Tanzania na Uganda.

Wakati wetu wa ama kutekeleza au kutelekeza wajibu wetu
Mwaka juzi kipindi watu wa Nigeria walipokuwa wakisherekea mafanikio ya miaka 50 ya jamhuri. Mwandishi wa vitabu vya Riwaya (marehemu kwa sasa) hayati Chinua Achebe, hakuwa na lolote lile la kusherekea, kutokana na adha ya uhuru aliyoipata mbali na kuwa mwasisi wa matunda hayo.
Akiongea na mwandishi wa habari Gwiji huyo alidai kuwa, Nigeria imewasonenesha na kuwahuzunisha wapendwa na marafiki waliokuwa wakiitakia amani na mafanikio makubwa.
Alisema miaka 50 ni muda mrefu, hasa kwetu sisi tuliokuwa watu wazima tayari.
Matarajio yalikuwa makubwa mithili ya maajibu. Lakini ajabu kubwa nililokwisha shuhudia ni ajabu la kukatisha tamaa. Alisema Chinua Achebe.
Ikumbukwe kuwa, mnamo octoba 1,1960, Nigeria ilipata uhuru wake toka kwa mwingereza ikiwa chini ya uongozi wa waziri mkuu, Alhaji Sir Abubakari Tufawa Balewa. Baadaye iliongozwa na Gavana wa shirikisho Dr Nnamdi Azikiwe, kama mwakirishi wa malkia wa Uingereza kabla ya oktoba mosi, 1963 kuwa jamhuri ya shirikisho ikiongozwa na Dr.Nnamdi Azikiwa kama Rais wa nchi hiyo.
Miaka 16 ikiwa chini ya utawala wa kijeshi kabla ya Rais Olusegun Obasanjo kuchaguliwa kidemokrasia hapo februari 1999. Nigeria imepita katika mapito ya tawala zisizowajibika kwa wananchi. Serikali ya Obasonjo ililazimika kutumia mamilioni ya fedha kutafuta akaunti za watawala tangulizi waliokuwa wameficha fedha ughaibuni(hasa gen. san Abacha) pamoja na kufumua upya lessen na mikataba iliyoonekana kutiliwa shaka kubwa na kuzidisha mapambano dhidi ya tabaka la watendaji katika serikali ili kufuta harufu ya urasimu.
Hata hivyo tangu Nigeria ya utawala wa kijeshi na baadaye utawala wa kidemokrasia wa Rais Olusegun Obasanjo na sasa Goodluck Jonathan bado imegubikwa na machafuko ya kijamii hasa yatokanayo na tofauti za kimtazamo kama vile Boko haram pamoja na siasa za chuki.
Sierra Leon baada ya kupokea uhuru kutoka kwa mwingereza mwaka 1961 chini ya chama cha Sierra Leon peoples part (SLPP) kiliongozwa Sir Milton Marngai kabla ya kupokezana kijiti na kaka yake Sir Albert Marngai hapo mwaka 1964 hakuna lolote lile lilotendeka kuashiria nchi kuwa huru
Sera za umiriki wa Aridhi zilizotungwa kwa misingi ya katiba mbovu iliyotengenezwa kwa maslahi ya walio wachache, za kuzuia kumiliki, kulima kahawa, kokoa wala kuuza aridhi kwa mtu asiye mwanamfalme au anatokea ukoo wa kichifu zilitosha kuwapasha habari watawaliwa juu ya aina ya uhuru walioupata. Mwaka 1967 ndipo walipoamua kuondoa utawala wa kichifu wa ukoo wa Marngai kwa njia ya demokirasia chini ya chama cha All people’s part(APP) kikiongozwa na Steven Siaka
Tafsiri ya siasa katika nchi nyingi barani Afrika ni kupata nguvu ya kiuchumi kwa mwanasiasa husika, familia yake, ukoo wake, ikiwezekana hata eneo atokalo. Mwaka 1970 Steve Siaka alitaifisha mgodi wa Almas kutoka kwa kampuni ya Debeers ya Afrika kusini na kuuweka chini ya umiliki wa serikali huku yeye mwenyewe binafsi akiwa anamiliki asilimia 50 ya hisa zote katika share.
Mwaka 1980, aliyekuwa Gavana wa Bank kuu wa nchi hiyo Samwel Bangura alibaini kile alichokiita mbinu chafu ya Rais ya uchotaji wa mamilioni ya fedha(takribani dola za kimarekani milioni 50). Fedha iliyokuwa imetolewa na Rais wa Libya wa wakati huo Muamar al – Qadaff kwa ajiri ya kufanikisha mkutano wa O.A.U. Bangura alikutwa amekufa nje ya nyumba yake siku chache baada ya kutoa tuhuma hizo. Kwa mjibu wa gazeti la majira la julai 28, 1980 linaripoti kuwa siku chache kabla ya mkutano wa O.A.U kuanza, polisi ilikamata vipeperushi vya gazeti la upinzani lililoweka wazi madudu yote kwa vithibitisho vya akaunti namba za wahusika. Jambo ambalo Steven Siaka alidai ni mchezo mchafu wa vijana wa mitaani.
Kwa Afrika, taasisi za kinyonyaji za kisiasa (extractive institututions) kama zilivyorithiwa kutoka kwa wakoloni, zimekuwa zikirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ndicho alichokifanya Steven Siaka, muda wake mrefu wa kukaa madarakani ulirithiwa na Joseph Momoh.
Ufedhuri na udharimu mkubwa juu ya wanyonge na wanawema wa Siera Leon uliotekelezwa na Joseph Momoh ndani ya muda mfupi ulitokomeza kabisa chembechembe za matumaini kwa wanawema hao mafukara wa Sierra Leon.
Aliyekuwa mtaalamu wa taaluma na tiba ya magonjwa ya akili na mpigania uhuru wa Algeria Frantz Omar Fanon aliwahi kusema kuwa ‘kila kizazi, katika changamoto za wakati wake, kina wajibu, aidha kiutekeleza ama kiutelekeze’.
Katika dhana ya kuutekeleza wajibu, wateswa na waathirika wa umasikini nchini Siera leon, waliwaunga mkono waasi wa kikundi cha RUF (Revolution United Front), ambao katika kupambana na manyang’au wa serikali ya nchi hiyo, waliingia wakitokea Liberia wakiwa na kaulimbiu ya “njia kuelekea demokrasia ya kweli”. Waasi hao walidai kuwa “tunapambana kwa kuwa tumechoka kuwa wahanga wa umasikini na uvunjifu wa haki za binadamu katika nchi yetu. Tutaendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuidai haki hadi pale kila mmoja wetu atakapokuwa mshindi.
Hadi leo watu wa sierra leon hawajawahi kushinda, kwani baada ya vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe masikini hao hadi leo wanataabika na njaa, ujinga na magonjwa ya hatari kama vile Ebola.
Tunapokumbuka migogoro iliyokuwa ikijitokeza katika vipande mbalimbali vya bara la Afrika, hatuna budi kukumbuka pia yale yote yaliyoisibu nchi yetu mara tu baada ya kupata uhuru. Katika kitabu chao cha miongozo miwili; Kupaa na kutunguliwa kwa Azimio la Arusha; Profesa Issa Shivji na wenzake wananukuu mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ukidai kuwa; mabadiliko makubwa ya mapato na hali ya maisha yalionekana kwa wachache, viongozi na Maafisa wa Chama waliokabidhiwa madaraka yaliyokuwa yanashikwa na wakoloni. Tafsiri ya hali hii ilijitokeza waziwazi wakati umma ulianza kuwaita wale walioonekana wanafaidika kwa vyeo vya uhuru “Naizesheni” wakati wananchi waliobaki waliitwa (Baba Kabwela).
Ndipo Mwl. Alipoona kuna haja ya kuweka misingi mipya na ya kimapinduzi ya kulijenga na kulilinda Taifa kupitia Azimio la Arusha na kuliweka hadharani.
Mwalimu kuonesha kwamba alikuwa hayuko tayari kuona nchi yake ikiingia katika migogoro itokanayo na misingi ya kimaslahi na ukiukwaji wa haki za Binadamu, aliamua kusimamia na kuiishi misingi ya Azimio la Arusha. Moja ya utekelezaji wake ilikuwa ni kutaifisha mabenki, biashara ya nje na mashamba makubwa ya mabepari, kuundwa kwa mashirika ya umma na kuanzishwa kwa viwanda vya umma ni baadhi tu ya mambo yaliyodhihilisha nia ya Mwalimu ya kuunda mfumo mpya wa uchumi unaofanana na jamii ya kijamaa inayodhaminiwa kujengwa. Jambo hili ndilo lililotofautisha historia ya kipande cha nchi yetu na vipande vingine katika bara la Afrika kama vile Nigeria, Siera leoni, Algeria, Zaire, Uganda n.k.
Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1990. Tanzania ikachutama na kusitiliwa na nguo mpya ya uliberali mamboleo. Kila jambo liliamliwa kwa jina la wahisani na wawezeshaji.
Tanzania ya leo, ni tofauti kabisa na ile ya Baba wa Taifa. Viongozi wamejisahau. Kujisahau kwao kumejenga na kuharalisha tabaka la walionacho na wasionacho. Matokeo ya matabaka haya yamejenga chuki baina ya walalahoi na walahai (vigogo).
Haya ni matokeo ya kushamili kwa rushwa katika nchi na imekuwa kama haki ya msingi kwa kila mwenye dhamana katika utumishi wa umma na / au Binafsi, kuomba na kupokea rushwa.
Katika kujenga tafakuri, ni lazima tuwe tunailinganisha Tanzania ya leo na ile ya wakati wa mwalimu, ambayo japo watu wake walikuwa mafukara lakini viongozi waandamizi wake hawakuwa matajiri kama viongozi wa leo. Azimio la Arusha lilimzuia kiongozi kuwa mfanyabiasha.Hivyo mwalimu hakuwaruhusu kutumikia mabwana wawili, kwani alijua fika kuwa mfanyabiashara huwa ana masilahi ya kudumu. Hofu yake aliijenga juu ya masilahi binafsi katika utungaji wa sera.
Lazima tujiulize kwa nini Tanzania hiyo ienda kombo, ikazame na kuibuka kuwa nchi yenye kupalilia ufisadi, yenye serikali iliyo na kashifa zisizokwisha kama vile za mikataba mibovu mfano wa Richmond, IPTL na Statoil. Tanzania yenye viongozi wenye akaunti nje ya nchi zenye harufu ya fedha za wanyonge kama vile za “EPA, rada, na za Tegeta escrow. Yenye viongozi walionona na bado wangali hawajatosheka.
Tunapoelekea katika kipindi cha kuipigia kura katiba ni lazima tujiulize iwapo itakuwa katiba yenye meno ya kuweza kuufyeka unyang’au uliopo. Tujiulize iwapo tunataka nchi ambayo wote tutaungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kurejesha ndoto na matarajio ya wanyonge na kujenga daraja la watu wenye kipato cha kati.
Ni lazima tujiulize iwapo itatuletea uchumi na uongozi imara unaoweza kufanya kazi kwa pamoja kwa dhamira ya kugawa fulsa sawa, wajibu, haki na maisha bora kwa kila mtanzania? Au tunatengeneza katiba itakayozaa serikali dhaifu na makundi imara ya kimasilahi yenye kuhakikisha yanamnyonya mnyonge hadi tone la mwisho?
Haya ni maswali ambayo kila mmoja wetu hasa vijana anapaswa kujiuliza. Huko ndiyo kuenzi na kuzihui fikra na yale yote ambayo Baba wa taifa alikuwa anayasimamia na kuyaishi, na kinyume cha hapo ni kupalilia yale yanayowasibu Wanigeria na watu wa Sierra leon kwa sasa. Idumu Tanzania, Idum Afrika
Mwandishi wa makala; Hoja lugalila; 0752900305,lugalilahoja@gmail.com