Monday, 2 May 2016

HEBU ZIFAHAMU SIFA ZA BINADAMU ANAYEJITAMBUA


Katika makala hii tunajifunza juu ya binadamu anayejitambua.Makala hii inaweza kukukumbusha mambo mengi kwa kifupi na hivyo kukufanya uchunguze juu ya maisha yako na kuyatumia vyema kwa wakati huu ulipo hapa duniani.


Kutambua ndani yako hakuhitaji uende shule na kusoma sana,na hakutokani na maamuzi ya mtu mwingine bali ni maamuzi yatokayo ndani mwako
Ni mguso unaotaka ndani mwako, ufahamu unaokua toka ndani mwako. Ni uchimbuzi wa chemchem zitokazo ndani mwako, Ni kumtambua Mungu kupitia mguso ndani ya moyo wako, kisha kuanza kutumia kipawa ulichonacho kwa ajili ya utukufu  wa Mungu . Ni hisia za ndani zitakazofanya umfahamu Mungu na si kufikiria tu.Upya ndani ya binadamu hutokea wakati wote  kwa kuunganisha moyo wako na ulimwengu wa hisia na kuendelea kujifunza kila wakati na kukuza nafasi ya moyo wako kuwa mpya.
 na
Je ni kwa namna gani unamtambua binadamu anayejitambua?

Mtu anayejitambua hubadili mtazamo wake kutoka kwenye mtazamo wa jamii unaofuata mila na desturi/kawaida kuelekea kwenye fikra za kuijenga dunia mpya na yenye fursa mpya.Hujenga dunia ambayo wanaomzunguka ni wanadamu wanaotambua utu na nafasi ya kila nafsi.Akiwa na misingi ya ujamaa na usawa, hufanya majukumu yake kutoka kujitazama yeye binafsi na kuanza kuwatazama wengine.Uchaguzi wake na matendo yake husukumwa na  maono na mtazamo wa mbali kwa ajili ya binadamu wote na viumbe vyote.Hutazama sio kila kiumbe kwa ajili yake,bali kila kiumbe kwa ajili ya wote.

Anayejitambua habagui jinsia bali hutambua jinsia kuwa ni matokeo ya fikra za Mungu yaliyokusuduia kutoa fursa.Huheshimu, hutambua wengine na kuthamini nafsi zao na uchaguzi wao.Hutengeneza dunia dunia ambayo jinsia zote huwa na uhuru wa  kutumia vipawa vyao, kutambua sauti zo,nuru ndani mwao na kutumia kwa ajili ya viumbe wote. 

Mtu anayejitambua hasukumwi kutenda na maamuzi ama fikra za wengine. Anatazama ndani yake.Hajifananishi na nafsi zingine na hivyo hatumii nafasi yeyote kuwakandamiza wengine.Husimama kwa miguu yake mwenyewe. Anawasikiliza wengine isipokuwa hatoi nafasi kwa wengine kumuamulia maisha atakayoishi. Anayaona mambo yajayo na hivyo huanza kuijenga kesho yake katika wakati tunaouita sasa. Ni alama ya uwezo wa Mungu uliopo ndani ya binadamu. Na alama ya maisha yake huishi enzi na enzi.

Mtu anayejitambua huchukua hatua juu ya hisia zitokazo ndani mwake na hivyo kutambua matokeo ya matendo yake.Hutenda kwa msukumo wa moyo. Hutambua mambo ambayo hayamletei faida na kutoyafanya na pia hutambua yale yanayomletea faida ..akitambua kuwa anapotenda kwa wengine anajitendea mwenyewe. Husikiliza hisia za ndani mwake na kujifunza lugha ya moyo wake.

Huishi maisha yenye sababu. Husikia muito alioitiwa na kuuuishi. Haridhishwi tu na maisha ya tokanayo na matukio kama kuamka,kutembea,kulala,kula bali hutambua kuwa yupo hapa duniani kwa sababu maalum,hivyo huchimba ndani mwake kuijua sababu na kuiiishi. Kila wakati anasukumwa na sababu hiyo  ya yeye kuishi ,kuendelea kuishi kwa dhati akitengeneza na  kuifuata njia inayomfikisha huko.

Hakimbii majukumu yake . Hajitoi katika kutafuta suluhu ya changamoto na wala halaumu wengine. Hutambua makosa yake na kujifunza kupitia hayo. Husanifu maisha yake na kuyafanya mapya kila wakati.
Hujifunza toka ndani mwake na kutoka kwa wengine. Hutilia mkazo katika mafanikio ya ukuaji ndani mwake kuliko mafanikio ya nje., hutengeneza ndani mwake. Hutafiti na kuvumbua chemchem zinazojenga na kubomoa nafsi na kutumia chemchem hiyo kuifanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.Hivyo aliyejitambua ni picha tosha ya uwezo na uwepo wa Mungu ndani ya binadamu. Hutengeneza msawazo kati ya chemchem ndani mwake na matokeo yaonekanayo halisia.;
Binadamu anayejitambua hutazama kila jambo kama fursa


Anayejitambua hatafuti usahihi katika utendaji bali hutenda kwa kujitolea katika nguvu na uwezo wote.Hufanya kwa uwezo wake wote.
Anayejitambua hujikita katika kutenda kuliko kusema tu.Huweka bidii katika kazi . Huanzisha na kutenda mambo ambayo hufaidisha viumbe wote . Husema pale inapohitajika,huheshimu mawazo yake na huwa tayari kuchukua malipo ya maneno yake mwenyewe.Hakimbii kivuli chake. Hayupo tayari kuona wengine wakikosa uhuru  kupitia yeye. Anatambua kuwa wakati wote huvuna alichopanda..

Anayejitambua huweka mkazo katika uhusiano mwema na nafsi zingine. Huthamini mahusiano yenye thamani. Mahusiano kwake hutokea ndani, hujengwa ndani na hivyo hudumu. Upendo kwake ni lugha ya moyoni, huleta furaha, mshikamano na amani.Zitokeapo changamoto katika mahusiano,huwa tayari kuyatatua kwa ajili ya kuyakuza zaidi.

Anayejitambua hutambua kuwa hapa duniani hatupo katika kushindana,ushindani kwake haupo,hushirikiana na ushindi kwake ni furaha katika kutimiza wajibu wake. Huandaa silaha zake ndani na kuteketeza kila kisicho na manufaa kwa binadamu. Baada ya milima na mabonde katika maisha yake ushindi huzaliwa ndani mwake. Hutumia uwezo wake kwa ajili ya Wengine na si dhidi ya wengine..

Huishi katika hali ya kujitolea na bidii. Huwa ni zawadi ya aina yake hapa duniani. Haogopi kutenda. Huendeleza mambo yaliyojenga utu,ubinadamu na misingi bora ya kuishi yaliyojengwa na binadamu waliomtangulia. Maisha yake hufundisha wengine.  Hutambua juhudi za wengine na wote wanaompa msukumo wa kutenda zaidi hasa pale anapokutana na  changamoto. Hutambua kuwa hayuko peke yake,bali dunia imejengwa kwa muungano wa nafsi zinazotimiza majukumu kwa dhati.

Haogopi ukweli hata pale unapoumiza. Hutoa nafasi ya kusamehe kila wakati anapokosewa. Hujisamehe yeye pia anapofanya makosa. Hushiriki katika ujenzi wa maisha yake.
Hutambua kuwa kila jambo hutoa fursa,kila kiumbe ana fursa. Hakusanyi ama kujilimbikizia kwa ajili ya sifa. Hutazama wengine kama anavyofanya kwa nafsi yake. Inapostahili hujitolea alichonacho,hutoa kwa wale walioshiriki kwa yeye kupata. Hutengeneza maisha yake yawe ya kutoa fursa kwa wengine badala ya kuwanyang’anya wengine .

Anayejitambua haichukuliai dunia kama chanzo cha maumivu bali hugundua kuwa dunia humpa kila mmoja kadiri anavyohitaji.Dunia husikiliza kutoka kwenye uwezo  ulio ndani mwetu tuliopewa na Mungu.Hata mara moja hajichukulii kuwa ni bora kuliko binadamu wengine na wala si dfhaifu kuliko wengine. Hutambua kushabihiana na kutegemeana kati ya kiumbe kimoja na kingine.Hivyo anatambua kuwa kama ikiharibu mazingira ,ni sawia na kuharibu nafsi yake.
Binadamu anayejitambua huyajenga na kuyatunza mazingira yanayomzunguka


Anayejitambua hamlaumu Mungu hata mara moja. Uhusiana wake na Mungu ni wa heshima,urafiki na huwa na umoja naye . Mienendo yake yote humwelekea Mungu .Anawaheshimu wanaoamini sawia naye na wasio amini sawia naye. Hashiriki kutumia imani ama dini kama njia ya  utengano kati ya binadamu,ama binadamu na mazingira yake.

Ni mfano wa sifa njema ya binadamu. Huchukua majukumu yake. Ana faida kwa viumbe wote.Hulinda, hujenga, huheshimu, Huishi vyema duniani. Ni mfano wa aliyeletwa kuifanya nuru ya Mungu ing’ae. Ni halisi,haishi maisha bandia. Ni wa kutumainiwa, si mbinafsi. Wakati wake kuwepo duniani ukifikia tamati,huondoka kwa furaha ya kutimiza alichotumwa,na kuacha dunia ikimlilia.Ni wewe na mimi.
- See more at: http://pongujoseph.blogspot.com/2013/09/sifa-za-binadamu-anayejitambua.html#sthash.JYyOmX8Q.dpuf