Saturday, 13 August 2016

NDOTO YAKO INAWEZEKANA

Lazima suala la kufanya mambo kwa ubora wa hali ya juu uwe sehemu ya maisha yetu na watu wengi sana huwa hawatumii muda wao mwingi kufanya mambo kwa ubora wa hali ya juu.Watu wengi wameshindwa kufikia hatima za maidha yao kwa sababu ya kushindwa kuwa bora sana kwa kile ambacho wanakifanya.
Ili ufikie kilele cha mafanikio yako ni lazima uwe mtu ambaye umeamua kufanya mambo kwa ubora wa hali ya juu sana bila kuchoka.Hivi umeshawahi kumtaja mtu mahali watu wakaanza kusema “Hapana,huyo hafai kabisa”.Swali ni kuwa je,wewe ukitajwa mahali kwa ajili ya jambo fulani watu watasemaje?.Siku zote watu hupenda kutoa fursa kwa wale ambao huwa wanafanya mambo kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu bila kujali wanafanya biashara,wanafanya kazi za taaluma zao ama za kutumia nguvu.
Ni rahisi sana kujua kama unafanya mambo kwa ubora ama la?Hivi nikikuambia kuwa nitakupa milioni tano leo kama utafanya kazi unayofanya sasa vizuri zaidi ya ulivyowahi kuifanya,je utafanya kwa ziada ama utafanya kama siku zote?Bila shaka ni kuwa utaongeza nguvu,akili na maarifa ya ziada katika kuifanya kazi yako.Kitu ambacho watu wengi hawajui ni kwamba fursa nyingi wamezizuia maishani mwao kwa kufanya mambo bila ubora.Kuna watu kila kazi utakayowapa lazima uirudie kuifanya mara mbili kwani wataifanya kwa kiwango cha hali ya chini tu.Kama wewe ni mtu wa namna hii basi ujue unajizibia mafanikio yako mwenyewe.
Kuna mambo Mawili unatakiwa kuyazingatia kama kweli unataka kufanikiwa kwa kufanya mambo kwa ubora wa hali ya juu:
Moja ni kufanya maamuzi kuwa wewe utakuwa mtu wa kufanya mambo kwa ubora bila kujali mazingira,malipo ama jambo lolote lile.Ili uweze kufanikiwa katika hili ni lazima uwe mtu ambaye ukiwa na jukumu la kufanya katika maisha yako ulifanye kwa asilimia 100.Kutofanya mambo kwa ubora ni mazoea tu wala sio kukosa uwezo.Hivi haujawahi kuona watu wanavaa hovyohovyo si kwa sababu hawana hela ila ni kwa sababu hawajazoea kufanya mambo kwa ubora.
Amua kuanzia leo kuwa chochote ambacho kitapita katika mikono yako basi ijulikane hivyo kwa sababu ya ubora wa kazi ambayo utakuwa umeifanya.Hebu jaribu kujichunguza leo-Kuna maeneo gani ya maisha yako ambayo watu wamekuwa wakilalamika kuwa haufanyi vizuri?Ukishayagundua hebu chukua hatua ya kuyarekebisha kwa kuanza kufanya mambo kwa ubora wa hali ya juu.Moja kati ya changamoto inayoweza kuzuia mafanikio yako ni ile hali ya watu kuhitimisha kuwa wewe ni mtu wa namna fulani;pengine huwa wanasema-“Yule kwa kawaida ni mchelewaji”.Kama kuna eneo la maisha yako watu kuna “ukawaida wako” wanausema basi namna nzuri sio kubishana nao bali ni kuanza kufanya tofauti na wanachosema hadi watakapoanza kukuona tofauti.
Jambo la pili ili kuishi katika kiwango cha ubora ni ile hali ya kila wakati kujiuliza mbinu mpya na bora zaidi ya kufanya ambacho unafanya kwa sasa hivi.Usikubali kufanya mambo kwa mazoea bila kutumia muda wa kujiuliza namna bor aya kufanya unachofanya kwa sasa.Mafanikio hutokana na kutumia muda wako kuboresha kile ambacho unakifanya.
Siku moja nilisikia habari ya mwanamke mmoja ambaye alikuwa kila siku siku akikaanga samaki huwa lazima amkate nusu kwanza.Sasa siku moja mtoto wake akamuuliza-“Mama hivi kwa nini kila siku unamkata samaki nusu,kwa nini haumkaangi akiwa mzima?”-Yule mama akasema “Hivi ndivyo bibi yako huwa anafanya siku zote na tangu nimezaliwa hatujawahi kukaanga samaki mzima”.Basi yule mtoto wa udadisi akaenda kwa bibi yake akamuuliza pia swali lile lile na akaambiwa-“Mimi nilimkuta mama yangu huwa anafanya hivi na miaka yote sijawahi kufanya tofauti”.Basi baada ya hapo mtoto aliamua kwenda kwa bibi yake akamuuliza tena swali hilohilo-naye akamwambia-“Mimi nilikuwa nakata samani nusu kwa sababu sufuria langu la kukaangia lilikuwa dogo samnaki mzima hakuweza kutosha”.Kumbe miaka yote hiyo watu wamekuwa wakifanya kitu ambacho hakina umuhimu na hawajui kuwa wangeweza kufanya kwa ubora zaidi.
Ndivyo ilivyo katika maisha-Kuna watu wengi sana ambao hufanya mambo kwa mazoea tu na hawajawahi kujiuliza kama wanachofanya kuna umuhimu wa kuendelea hivyo ama wanaweza kubadilisha kitu.Acha na tabia ya kufanya biashara kwa mazoea,acha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea-Kila wakati jiulize,hivi kuna njia gani bora ya kufanya hiki nifanyacho?
Leo hebu jaribu kutumia dakika chache kufikiria ni njia gani bora unaweza kuzitumia ili kufanya kwa ubora zaidi kile ambacho unakifanya sasa.Kumbuka kuwan kama ukiamua kutumia muda kufikiria kidogo tu utapata njia bora zaidi kuliko unayotumia sasa.Fikiria njia bora ya kufanya biashara yako na usitumie uzoefu,fikiria njia bora ya kufanya kazi yako na usitumie uzoefu.
Kumbuka kuwa ndoto yako inawezekana,