Friday, 20 May 2016

Mwanamke, Hata wewe unayo haki ya kutoa talaka...!!


 1. [​IMG]


  Kuna idadi kubwa ya wanawake ambao wanakaa kwenye ndoa wasizoridhika nazo, ndoa zenye kuwafuja na kuwatesa, ambazo kwao zimepoteza maana na hawana sababu ya msingi kuishi humo. Lakini wanawake hao wamejikuta wakiendelea kuishi ndani ya ndoa hizo kwa hofu tu.

  Wamekuwa wakiogopa kudai talaka kwa kudhani kwamba, wao hawapaswi kuomba talaka, bali wanaume ndio wanaopaswa kufanya hivyo na pia wamekuwa wakiamini kwamba, mwanamke kuanza kuomba talaka ni aibu kwa jamii.
  Lakini mbaya zaidi ni ile hofu wanayokuwa nayo kuhusu kile ambacho wanaume zao wanaweza kuwafanyia wanapoomba talaka. Huhofia kwamba, kama wanaume hawaridhiki na wao kuomba talaka, wanaweza kuwafanyia vitendo viovu baada ya talaka.

  Huogopa kwamba, wanaweza kuwanyang’anya watoto, huogopa kwamba, wanaweza kuwafanyia fujo kila watakapokutana nao, huogopa kwamba, hawataweza kuwagawia mali waliyochuma pamoja na pia kuna hofu kwamba, wanaweza kuwauwa, hasa ikiwa ni juhudi ya kuzuia uwezekano wa kuja kugawana mali.

  Ukweli ni kwamba, wanawake hawa wanapaswa kujua kwamba, wao hawawezi kujua vipengele vingi au vyote vya kisheria. Kwa sababu hiyo, wanapohisi kwamba, hawawezi tena kuvumilia vurugu za kindoa zinazowakabili, wanapaswa kuwaona wanasheria ili kuyaendesha mambo kisheria zaidi.

  Kama hawana uwezo kifedha, siku hizi kuna taasisi zinajua namna ya kuwasaidia wanawake hawa, hata kama hawana uwezo. Taasisi kama TAWLA au WLAC zimekuwa zikifanya kazi hiyo kwa muda mrefu sasa na zimesaidia wengi.

  Kwa hiyo badala ya mwanamke kuumia kwenye ndoa ya mateso kwa kutojua afanye kitu gani, anaweza kuwaona wataalamu wa sheria kutoka katika taasisi kama hizo au kutoka kwa wanasheria binafsi. Hawa wanajua hata namna ya kumfanya mwanaume mkorofi ambaye baada ya kupewa talaka anaweza kuwa kama mbweha badala ya binadamu, ajirekebishe na kufuata sheria za nchi.

  Kukaa kwenye ndoa kwa sababu mwanamke anaogopa mabavu ya mwanaume ni dhana ya kale sana. Inabidi ifikie mahali ambapo mwanamke yuko huru kuanzia ndani mwake (Mawazoni na nafsini) hadi nje. Mwanamke anapaswa kujua kwamba, wakati mwingine hafungwi na mwanaume, bali hujifunga mwenyewe…….