Monday 30 May 2016

Faida tele wanaume kufua, kwenda kliniki

KUONA baba akiwa ameandamana na mkewe kliniki, kuona baba akifua au kupika huku mama akifanya shughuli nyingine, inaelezwa kwamba ilikuwa ni mwiko katika jamii ya Wafipa, mkoani Rukwa.
Hali hiyo ya mwanamke kufanya kila shughuli haikuwa miongoni mwa watu wa vijijini pekee, bali hata ‘wasomi’ kama walimu, madaktari, waratibu wa elimu na wengine kama hao. Kundi la waandishi wa habari waliotembelea katika maeneo ambayo Mradi wa Ushiriki Sawa wa Wanaume katika Afya ya Uzazi na Ujinsia (TMEP), ulikuwa unafanyika kwa kipindi cha takribani miaka mitano, waligundua mabadiliko chanya yaliyoletwa na mradi huo.
Hata hivyo, mradi huo ulikoma mwishoni mwa mwaka jana, lakini mafunzo yaliyopatikana yanapaswa kuendelezwa. Uso kwa uso mwanamume akifua Waandishi wakiwa katika kijiji cha Nkana, kata ya Sintai wilayani Nkasi, mkoani humo, walimkuta Petro Evodi Pahali akifua nguo zake na za mkewe, huku mkewe huyo akiendelea na shughuli zingine za kutayarisha chakula cha familia.
Alipohojiwa akiwa uani mwa nyumba yao ya matofali ya kuchoma, Pahali ambaye mwaka huu amefikisha umri wa miaka 31, alisema tangu ashiriki mafunzo yaliyokuwa yanatolewa na mradi wa TMEP yamemhamasisha kubadilika na sasa anafua nguo zake mwenyewe na za mkewe na wakati mwingine kusaidia shughuli za nyumbani kama vile kupika na usafi wa nyumba kadri anavyopata nafasi.
“Kabla ya hapo kwa kweli nilikuwa siwezi kufua hata kama sina kazi. Hii ilikuwa ni shughuli ya mke wangu. Lakini siku hizi ninafua na wakati mwingine mtoto akiumwa nampeleka mwenyewe zahanati,” anasema Pahali ambaye ni mkulima na Katekista katika kijiji hicho, yaani mwalimu wa dini. Pahali, baba wa watoto wawili, anasema kwa vile mkewe kwa sasa ni mjamzito, yeye ameamua kumsaidia majukumu kadhaa ikiwa ni pamoja na kufua.
“Lingine ninalolifanya ni kwamba kila akienda kliniki lazima tuandamane pamoja. Hii ni tofauti na zamani ambapo wakati wa ujauzito wa watoto wangu hawa wawili na hadi kuzaliwa kwao sikuwahi kuandamana na mke wangu hospitali. Kwa kweli sasa ndio ninagundua kwamba ule utaratibu wetu wa zamani... mnaita mfumo dume eh... ulikuwa ni utesaji,” anasema.
Pahali anakiri kwamba mila zao za Kifipa hazikuruhusu mwanamume kufanya shughuli zilizoonekana kama za kike kama kupika, kufua na masuala ya kulea watoto ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kliniki. Anasema tangu elimu ya ushiriki sawa wa wanaume katika haki ya uzazi na ujinsia ifike kijijini hapo, wanaume wengi wamebadilika na ni wachache wanaoendelea kumuona mwanamume anayefanya kile kilichozoeleka zamani kwamba ni kazi za kike kama mtu aliyetawaliwa na mkewe.
Lakini kubwa anasema tangu aanze kumsaidia mkewe shughuli mbalimbali, mapenzi motomoto yameongezeka sana baina yake na mkewe. Mkewe, Regina Papala, anakiri kwamba zamani mumewe alikuwa hamsaidii kazi za nyumbani hata kama anaumwa au ana ujauzito wa kujifungua, labda ikibidi ataita dada zake kumsaidia lakini si yeye kuzifanya kama vile kuingia jikoni kupika kama ilivyo siku hizi.
“Alivyoanza kwenda huko kwenye huo mradi, hata sijui unaitwaje, ndipo akawa anabadilika taratibu. Ninashukuru kweli siku hizi ananisaidia na hasa hivi nilivyo mjamzito,” anasema. Hata hivyo, Regina aliyezaliwa mwaka 1988 anakiri kwamba baadhi ya wifi zake wanaona kama sasa anamtawala mumewe. “Kuna wengine wakiona ananisaidia kazi za nyumbani wananiuliza, ‘kwa nini mumeo anafua, anapika wakati wewe upo?’
Mimi ninawaambia ‘ndwile’ (ninaumwa),” anasema na kuongeza kwamba huwa anaamua kusema hivyo ili kupunguza maswali. Maofisa tiba kubadilika Waandishi pia walipotembelea katika Kituo cha Afya cha Kirando, wilayani Nkasi ambapo, pamoja na kufanya mahojiano na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk William Msinjili, walitembelea eneo la kliniki pia, walikuta wanawake wengi wakiwa wameandamana na waume zao.
Dk Msinjili ambaye pamoja na maofisa kadhaa wa tiba wa kituo hicho walipata mafunzo kuhusu ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa TMEP anasema mradi uliwasaidia sana kupata mbinu za kuwahamasisha wanaume kuandamana na wake zao kuja kliniki. Dk Msinjili anashukuru mradi wa TMEP kuja na mtazamo tofauti ambao umesaidia kwa kiwango kikubwa kubadilisha mitazamo ya maofisa tiba na wananchi kwa ujumla.
“Jamii na hata sisi madaktari, zamani tuliona kwamba, kwa kuwa mwanamke ndiye anayezaa, basi kila kitu tulikuwa tukimwambia au kumfundisha yeye kama mlengwa, kumbe tulikuwa tunakosea. Tulisahu kwamba katika jamii yetu yenye mfumo dume, na hasa huku Ufipani, baba ndiye mtoa maamuzi na hivyo akielewa yaye basi mambo mengi yanakwenda kama tunavyotarajia,” anasema.
Anasema huko nyuma kabla ya mradi, ilikuwa inatokea mama mjamzito anagundulika kuwa ana matatizo au anatakiwa kujifungua katika uangalizi mzuri zaidi na ikiwezekana kupelekwa katika hospitali kubwa, lakini kwa vile baba hahusishwi katika kupata taarifa hizo kutoka kwa daktari aliweza kupuuza. Anasema kupuuza huku wakati mwingine kulisababisha madhara makubwa kwa akinamama wajawazito ikiwa ni pamoja na vifo.
“Yaani ilikuwa shida, baba anakataa hata kununua baby shawl (nguo nzito maalumu ya kubeba mtoto),” anasema na kuongeza kwamba baada ya elimu kusambaa tatizo kama hilo limepungua sana. Anasema kwa vile wanaume sasa wanahamasishwa kuja kliniki na wao ndio wanamiliki uchumi katika familia nyingi, wanalazimika pia kutafuta usafiri kama wa baiskeli au pikipiki.
“Zamani unakuta mwanamke ni mjamzito lakini anakuja kliniki kwa mguu, wakati mwingine kutoka kijiji cha mbali sana na mumewe hajali. Lakini kwa kuwa sasa hivi wamehamasika kuja pamoja, unakuta wanaume hawa mara nyingi wanaandaa pia usafiri hususan kuwaleta wake zao wajawazito kwa baiskeli,” anasema.
Ingawa alisema hakuwa na takwimu sahihi wakati waandishi walipomtembelea ofisini kwake, Dk Msinjili alisema vifo vya akinamama wajawazito na watoto vimepungua sana katika kituo hicho na yeye anaamini hali hiyo imeachangiwa kwa kiasi kikubwa na mradi wa TMEP.
“Sikuandaa takwimu lakini mkija siku nyingine mtazikuta... Vifo vya akina mama na watoto kwa kisi kikubwa vimepungua,” alisema. Uso kwa uso na wanaume kliniki Waandishi walipotembelea eneo la kliniki ya wazazi kituoni hapo, walikuta wanaume kadhaa wakiwa wameandamana na wake zao na baadhi walikuwa wakishiriki vipimo mbalimbali sambamba na wake zao.
Miongoni mwa wanandoa waliozungumza na waandishi wa habari kituoni hapo ni pamoja na Venance Mabuta aliyekuwa na mkewe, Amina Saidi na Athanas Kauzeni aliyekuwa ameandamana na mkewe mjamzito, Christina Kasangala. Wote walikiri kwamba zamani haikuwa rahisi mwanamume ‘kuacha shughuli zake’ na kwenda kliniki kwa kuwa waliamini hilo ni jukumu la mwanamke ambaye ndiye anabeba mimba na kisha kujifungua.
Akizungumza na waandishi wa habari, Athanas Kauzeni alikiri kwamba mfumo wa sasa wanaume kuandamana na wake zao katika kituo cha afya ni mzuri kuliko zamani wanawake walipokuwa wakienda peke yao. Anasema kupitia mfumo huo, yeye na mkewe hukaa na maofisa wa tiba na kujua kwa pamoja kama kuna tatizo lolote ili kulikabili pamoja na kujua ni nini waandae kabla ya mtoto kuzaliwa. “Kwa mfano, mke wangu hatakiwi kufanya kazi nzito.
Kama hili angeliambiwa peke yake huku mimi nikiwa sipo, ningedhani anataka tu kulala kwa kusingizia ujauzito lakini hapa ninapoambiwa na wataalamu basi ninajua ni kweli, si ujanja ujanja wake,” anasema. Katika kliniki hiyo ya mama, baba na mtoto katika kituo cha afya cha Kirando waandishi walizungumza pia na mmoja wa akinamama ambaye hakuwa ameandamana na mumewe.
Huyu ni Grace Ngoloka aliyekuwa na watoto wawili akisema kwamba mumewe hajahamasika vya kutosha kumsindikiza yeye na watoto kliniki kama ilivyo kwa wengine. “Mume wangu ni mkulima lakini tofauti na wengine haoni kama anapaswa kunisaidia kuja kliniki na hawa watoto wawili,” alisema.
Kituo cha Afya Kirando kilianza kazi mwaka 1974 kama zahanati na siku hizi kinahudumia maeneo mengi ya wilaya ya Nkasi kama Kabwe, Kolongwe, Namasi, Kaluya, Kisambala na hata wakati mwingine Wampembe. Hali kama hiyo ya wanaume kusindikiza wake zao kliniki au kupeleka watoto kliniki bila wake zao ilionekana pia katika Kituo cha Afya cha Matai wilayani Kalambo.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho ambacho wakati waandishi wanatembelea kilikuwa mbioni kuwa Hospitali ya wilaya ya Kalambo, Richard Mafunda, alisema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la akina baba kuandamana na wake zao hospitalini kuliko zamani kabla mradi wa TMEP haujawafumbua macho wanavijiji. Anasema mwaka jana walifikia asilimia 100 ya wanaume kuandamana na wake zao kliniki tofauti na zamani ambapo ilikuwa asilimia chini ya tano.
“Pamoja na elimu, lingine linalohamasisha wanaume kusindikiza wake zao kliniki ni kwamba kila mama anayekuja na mumewe, anapewa kipaumbele cha kuhudumiwa kwanza kulinganisha na wale wanaokuja bila waume zao. Mmoja wa wanaume aliyekuwa ameandamana na mkewe katika kituo hicho cha afya cha Matai ni Leonard Kasanda na mkewe, Huruma Masumbuko.
Kasanda alisema pamoja na kuelimika kwamba ni muhimu kusindikizana na mkewe mjamzito kliniki, lakini anashukuru utaratibu wa zahanati hiyo wa mwanamke anayeandamana na mkewe kupewa kipaumbele cha kutibiwa kwanza. Mradi wa Ushiriki sawa wa Wanaume katika Haki ya Afya ya Uzazi na Ujinsia (TMEP) ulikuwa unafadhiliwa na Taasisi ya Elimu ya Afya na Ujinsia ya Sweden (RFSU) na kuendeshwa katika mikoa ya Rukwa na Singida.
Mradi huo sasa umekoma na kuacha maswali baada ya kuleta mafanikio makubwa. Mradi huo umekuwa ukimlenga mwanamume kama chanzo cha mabadiliko katika jamii ambapo unaamini kwamba, yeye kama mtoa maamuzi katika jamii nyingi akielimika basi suala la afya ya uzazi linakuwa jepesi. Je, nani ataendeleza elimu hii katika mikoa mingine ili kuwazindua wanaume washiriki sawa na wake zao katika kila jambo?
Na je, Rukwa na Singida waliopata elimu kupitia mradi huu wataendeleza waliojifunza? unatarajiwa kufikia ukomo mwishoni mwa mwaka huu na kwa sasa umekabidhiwa kwa wananchi na halmashauri za miji na wilaya mkoani Rukwa ili uwe endelevu.

No comments:

Post a Comment