Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Anna Mghwira |
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Anna Mghwira amesema umiliki wa ardhi kwa wanawake hapa nchini bado unasuasua kutokana na mfumo dume uliopandikizwa tokea miaka ya nyuma.
Bi Mghwira ambaye alikuwa mwanamke pekee aliyegombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015 kupitia ACT Wazalendo, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Blogs za Mikoa kuhusu sababu za wanawake wengi nchini kutomiliki raslimali muhimu ya ardhi.
Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 idadi ya wanawake hapa nchini ni asilimia 51% lakini wanaomiliki ardhi ni asilimia 19% tuu jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa wanawake wengi bado hawamiliki ardhi ukilinganisha na wanaume.
''Tatizo lililopo hapa nchini ni tatizo la kitamaduni, ilikuwa kazi ya mwanamke akishazaliwa ni alelewe na baadaye akiolewa anaendeleza kizazi huko alikoolewa lakini kumiliki ardhi ni mfumo mpya ambao unatoa fursa sawa katika kumiliki raslimali hiyo muhimu kwa ajili ya kuitumia katika shughuli za kiuchumi,' aAmesema Mghwira.
Bi Mghwira ameenda mbali zaidi na kuona tatizo la umiliki wa ardhi pia lipo kwa upande wa wanaume hasa inapotokea suala la makubaliano na mwekezaji ndiyo maana kuna kesi nyingi kuhusiana na wawekezaji na wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Katika jitihada za kuunga mkono Serikali katika jitihada mbalimbali za kutatua kero kwa wananchi Bi Mghwira amesema kwamba mara kwa mara amekuwa akielimisha wanawake hapa nchini katika kutambua haki zao na kujikwamua na umasikini.
Hata hivyo ameitaka serikali kutizama upya sheria ya ardhi na pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umiliki wa ardhi ili kuwezesha wananchi kutambua kuwa umiliki wa ardhi ni wa haki kwa pande zote kwa upande wa wanaume na wanawake.
No comments:
Post a Comment